Mbunge Mafuwe aiomba Serikali kuingilia kati ufujaji wa fedha kiwanda cha kukoboa mpunga
Muktasari:
- Mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe ameiomba serikali kuwachunguza wakandarasi waliokuwa wakitekeleza miradi ya kiwanda cha kukoboa mpunga cha Mijongweni na Kikavu chini iliyogharimu zaidi ya Sh790 milioni kwa kushindwa kuikamilisha miradi kwa miaka minane tangu ilipoanzishwa.
Hai. Mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe ameiomba serikali kuwachunguza wakandarasi waliokuwa wakitekeleza miradi ya kiwanda cha kukoboa mpunga cha Mijongweni na Kikavu chini iliyogharimu zaidi ya sh.790 milioni kwa kushindwa kuikamilisha miradi hiyo na kuitelekeza.
Mafuwe ameyasema hayo leo Februari Mosi wakati alipofanya ziara ya kwenda kuikagua miradi hiyo akisema haijatekelezwa licha ya kutengewa fedha nyingi za serikali kwa miaka minane mpaka sasa.
“Tayari kuna zaidi ya Sh790 milioni za serikali ambazo zimelala hapa kwa miaka mingi ,wakati wananchi wanataka mradi huu uweze kuwaokoa na kuwakomboa kwenye umaskini na hiki ndicho kilio cha Rais wetu Magufuli (John) kwamba serikali yake ina tazama watu wanyonge, lakini wapo watu hawana nia njema na miradi.
“Nimwombe Waziri wa Tamisemi atume watu kwa haraka waje wachunguze miradi hii ikiwa ni pamoja na Takukuru, maana fedha ambazo ziko chini ni nyingi mno, ninaomba hili jambo lishugulikiwe kwa uharaka ili wananchi waweze kunufaika na miradi hii ambayo inatolewa na serikali,” amessema Mafuwe
Pia, amewataka wananchi pamoja na serikali ya kijiji kuhakikisha wanaendelea kulinda rasilimali zilizopo katika miradi hiyo mpaka pale serikali itakapokuja na muafaka mwingine juu ya miradi hiyo.