Mchungaji KKKT adai Dar es Salaam, Pwani kuna manabii wa uongo

Mkuu wa jimbo la kati Dayosisi ya Magharibi Kati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baraka Mungure

Muktasari:

  • Mkuu wa jimbo la kati Dayosisi ya Magharibi Kati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baraka Mungure amesema mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ina baadhi ya manabii ni waongo na wanasaka  fedha  za watu badala ya kuponya mioyo yao.


Dar es Salaam. Mkuu wa jimbo la kati Dayosisi ya Magharibi Kati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baraka Mungure amedai mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ina baadhi ya manabii ni waongo na wanasaka fedha  za watu badala ya kuponya mioyo yao.

Mungure ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 7, 2022 wakati akihubiri kwenye ibada ya kwanza ya katika kanisa la Azania Front mkoani Dar es Salaam.

Kabla ya kutoa ujumbe huo, mahubiri yake yalijengwa katika msingi wa maagizo ya Mungu kupitia biblia takatifu, Yeremia sura 23:16-22 (waumini wa Kikristo), ujumbe unaosema; Bwana wa Majeshi asema hivi, msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria, kuwafundisha ubatili, hunena maono ya mioyo yao, ambayo hayakutoka katika kinywa cha bwana. Tazama tufani ya bwana, yaani ghadhabu yake imetokea, ni dholuba ya kisulisuli, itapasuka na kuwaangukia waovu kichwani. Hasira ya bwana haitarudi. Siku za mwisho mtalifahamu hilo neno, mimi sikuwatuma manabii hao lakini walikwenda mbio, sikusema nao lakini walitabiri.


Katika ufafanuzi wake, kiongozi huyo wa Kanisa Kuu la Tabora amesema jamii imeendelea kuwa na maswali mengi kuhusu mitume na manabidii wanaotengeneza na kuuza mafuta na vitambaa.

“Kuna bodaboda leo amenibeba asubuhi akaniuliza mtumishi mbona siku hizi mnaweka mkazo sana kwenye mafuta na vitambaa? Halafu wanaowaponya Ukimwi anawafunika uso?”

“Nilitafakari sana maswali yake. Kwa sehemu kubwa Dar es Salaam na Pwani wamekubwa na hali hii, wanawake ndio wamekuwa wahanga wakubwa.  Watu wanajiuliza kwanini wasianzishe huduma hiyo huko Tabora vijijini wanakohitaji neema zaidi? Ila wao wako mijini tu ili wajinufaishe,” amesema.

Amebainisha kuwa kazi kubwa ya manabii zamani ilikuwa  kuonya, kukemea watu kuacha dhambi na kueleza ghadhabu ya Mungu.

“Lakini leo hii kama wanacheza na saikolojia zetu wakiona kuna tatizo fulani kwenye jamii ndio wanalolitumia, akina mama ndio wahanga zaidi.”

“Baadhi wanaoshawishika baadaye wanakuja kujutia maumivu. Hii inatukumbusha juu ya manabii wa uongo, ndugu zangu nabii wa mwisho ni Yesu katika familia yako,uchumi na maisha yako. Hatuhitaji tena manabii wasioshughulika na roho zetu ila wanashughulika na pochi zetu,”amesema.