Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchungaji Malisa matatani, ashitakiwa kwa uhaini

Muktasari:

  • Kesi hiyo iliyopangwa kutajwa kesho Ijumaa Januari 2, 2026, ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Dar es Salaam. Mchungaji Godfrey Malisa aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kufukuzwa uanachama mwaka jana, ameshitakiwa kwa kosa la uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Kesi hiyo iliyopangwa kutajwa kesho Ijumaa Januari 2, 2026, ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama wa Mahakama hiyo mkoani Kilimanjaro.

Hadi kufikia kesho, kesi hiyo iliyofunguliwa Desemba 2, 2025 Mchungaji Malisa atakuwa amefikisha siku 30 mahabusu.

Mchungaji Malisa amefunguliwa kesi hiyo ya jinai namba 000028333 ya 2025 chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Novemba 16, 2025 huko eneo la Miembeni katika Wilaya ya Moshi, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitenda kosa hilo la uhaini.

Inadaiwa alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kushiriki katika kusanyiko lisilo halali kwa lengo la kumtisha mtendaji wa Serikali ya Tanzania na alidhihirisha nia hiyo kwa kitendo chake cha kutamka na kuchapisha maneno yafuatayo;-

“Samia Suluhu Hassan…Kabla ya kufika tarehe 9 Desemba uwe umekwishajiuzulu… Kama utang’ang’ania madaraka itakapofika tarehe 9 Desemba kutakuwa na maandamano ambayo hayajawahi kutoka katika Bara la Afrika.”

Mchungaji Malisa anadaiwa kunukuliwa akisema: “Lengo la maandamano ni kumuondoa Samia Suluhu Hassan madarakani na maandamano hayo yatakuwa ni maandamano ya muendelezo mpaka utakapotoka madarakani.”

Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kosa hilo linaloangukia kifungu hicho cha 39(2)(d) ni kosa la uhaini kwa mujibu wa kifungu hicho.

Kifungu hicho kinasema mtu yeyote mwenye utii kwa Tanzania, endapo anaitisha Serikali na kubainisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi au machapisho au kwa kitendo chochote cha siri kinachojionesha cha hali yoyote, atakuwa na hatia ya kosa na endapo atatiwa hatiani atawajibika kwa adhabu ya kifo.

Mchungaji Malisa anaingia katika orodha ya mamia ya Watanzania walioshitakiwa kwa kosa la uhaini, iwe kwa kuchapisha maandishi au kushiriki katika maandamano ya Oktoba 29, 2025 ambayo Serikali iliyatangaza ni haramu.

Baadhi ya washitakiwa walifutiwa mashitaka na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) baada ya kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashitaka dhidi yao chini ya Kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hiyo ni baada ya Rais Samia kuielekeza ofisi ya DPP, kuwafutia makosa vijana wote walioonekana kushiriki maandamano ya Oktoba 29, 2025 kwa kufuata mkumbo, maandamano yaliyosababisha vurugu, vifo na uharibifu wa mali.

Rais alitoa kauli hiyo Novemba 14, 2025, katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 13 Mjini Dodoma akisema ukiangalia video za vurugu hizo, wapo vijana walioingia kwa mkumbo na walikuwa hawajui walitendalo.


Mchungaji Malisa ni nani

Mchungaji Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na mwaka 2015, aligombea urais kupitia Chamacha Kijamii  (CCK) na baadaye kugombea uspika.

Mwaka 2018 aligombea ubunge Kinondoni kupitia TLP na mwaka 2020 aligombea ubunge Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama cha NCCR- Mageuzi na baada ya uchaguzi ule alijiunga na CCM hadi mwaka 2025 alipotimuliwa.

Mwaka 2022 Mchungaji Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa  miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.

Hata hivyo, Februari 10, 2025 Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga uamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.

Uamuzi wa kumfukuza uanachama ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel akiegemea uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.

“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Januari 19, 2025,” alieleza Mollel.

Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba jambo ambalo si la kweli.

Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa kisha alihamia katika mitandao ya kijamii kuendelea kupinga uteuzi huo.