Meya Moshi ataka uchunguzi kampuni zisizopeleka michango NSSF
Muktasari:
- Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu amemwagiza meneja wa NSSF Mkoa wa Kilimanjaro, Large Materu kuzichunguza hospitali binafsi pamoja na kampuni zisizowasilisha makato ya wafanyakazi wao kwenye shirika hilo.
Moshi. Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu amemwagiza meneja wa NSSF Mkoa wa Kilimanjaro, Large Materu kuzichunguza hospitali binafsi pamoja na kampuni zisizowasilisha makato ya wafanyakazi wao kwenye shirika hilo.
Amesema mbali na hospitali hizo kutopeleka fedha za makato, amedai haziwatendei haki wafanyakazi wake wanapoumia kazini.
Raibu ametoa agizo hilo leo Jumanne Aprili 13, 2021 baada ya kupata malalamiko ya wafanyakazi kutoka moja ya hospitali ya manispaa ya Moshi.
"Nilipata malalamiko kutoka hospitali binafsi pamoja na mashirika ambayo yamekuwa hayawatendei haki wafanyakazi wake kinyume na taratibu na sheria za ajira, pamoja na kutopeleka fedha za wafanyakazi wao NSSF.”
"Nimemwelekeza meneja wa NSSF Mkoa wa Kilimanjaro , kuzichunguza Hospitali zote pamoja na kampuni binafsi ndani manispaa ya Moshi ambazo hazipeleki makato ya wafanyakazi wao NSSF ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema.