Meya wa Moshi aapa kupambana na makandarasi wa barabara
Meya wa Manispaa ya moshi, Juma Raibu akizungumza wakati wa mahojiano na Mwananchi digital leo.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu amesema atakula sahani moja na makandarasi watakaofanya kazi chini ya kiwango ndani ya Manispaa hiyo ambapo amesema tayari Serikali imetenga zaidi ya Sh1 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya barabara kwa kiwango cha moramu na lami.
Moshi. Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu amesema atapambana na makandarasi watakaofanya kazi chini ya kiwango ndani ya Manispaa hiyo, akibainisha kuwa tayari Serikali imetenga zaidi ya Sh1bilioni kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya barabara kwa kiwango cha moramu na lami.
Raibu ameyasema hayo leo, Agosti 30, 2021 wakati akizungumza na Mwananchi digital ofisni kwake, ambapo amesema kata zote 21 za Manispaa hiyo zitakarabatiwa na tayari makandarasi wako kwenye maeneo yao ya kazi.
“Tayari makandarasi wako maeneo ya kazi kwenye kata zote 21 kuhakikisha kata zote hizo barabara zinatengenezwa kwa kiwango cha moramu pamoja na lami,na tayari tumeshapokea fedha zaidi ya Sh500 milioni na kazi zimeshaanza kufanyika,” amesema Raibu
Ameendelea kusema kuwa katika matengenezo hayo hatarajii wala kuona mkandarasi kufanya kazi chini ya kiwango.
"Nitawachukulia hatua kali makandarasi wote watakaokwamisha shughuli hii.
“Nikibaini yupo mkandarasi yoyote ndani ya Manispaa ya Moshi amefanya kazi chini ya kiwango nitamchukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kupiga marufuku kutokufanya kazi sehemu yoyote ndani ya Manispaa hii ya Moshi," ameongeza.