Mfahamu IGP mpya aliyesifiwa na Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi Camillus Mwongoso Wambura baada ya kumwapisha kuwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) katika Hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo Jumatano Julai, 2022. Picha na Ikulu

Muktasari:

Pengine umewahi kumsikia Camilius Wambura, lakini usifahamu undani wa safari yake katika Jeshi la Polisi hadi kuwa IGP, hii ni historia yake.

Dar es Salaam. Pengine umewahi kumsikia Camilius Wambura kama kamanda wa Jeshi la Polisi, lakini usifahamu undani wa safari yake katika jeshi hilo.

Wambura leo Jumatano, Julai 20, 2022 ameapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Inspekta wa Jeshi la Polisi (IGP) akichukua nafasi ya Simon Sirro.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nafasi ambayo sasa imechukuliwa na Ramadhan Kingai.

Wadhifa wa DCI aliukwaa Mei 31, 2021 ikiwa ni siku 14 tangu aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Simon Sirro amuhamishie kuwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kutoka Mkuu wa Uendeshaji Upel Dodoma.

Uteuzi wa Wambura kuwa DCI ulitanguliwa na kupandishwa cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi hadi kuwa Kamishna wa Polisi ambapo jana Jumanne alipandishwa tena na kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Hata hivyo, Wambura alihamishiwa Dar es Salaam kuwa Kamanda wa Kanda hiyo Maalum, siku chache baada ya Rais Samia kusifu utendaji wake hasa katika kudhibiti matukio ya ujambazi katika Jiji hilo na kutaka arejeshwe jijini humo.

Katika hotuba yake alipokuwa akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam Mei 7, 2021, Samia amesema, “Tumeahidi kudumisha amani na usalama, kama wazee mlivyotuomba na hili tutasimia kwa nguvu zote.

“Leo nimesoma habari sio kwenye mitandao ya kijamii, wanajaribu kina cha maji, Dar naomba nitoe meseji wasijaribu kina cha maji na katika mitandao ile kuna Kamanda ametajwa kuwa alikuwepo hapa Dar lakini ameondolewa,” amesema.

Kabla ya nafasi hizo Wambura amewahi kuwa Mkuu wa upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam mwaka 2019, pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni mwaka 2018.