Mfumo mpya kukagua uzito wa magari Mikumi, Mikese wafikia asilimia 80

Morogoro. Mfumo mpya wa kukagua uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo katika mizani ya Mikumi na Mikese mkoani Morogoro umefikia asilimia 80 ambapo Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) umeeleza kuwa mfumo huo utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika mizani hiyo.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Morogoro Mhandisi Musa Kaswahili akizumgumza na Mwananchi Digital amesema matengenezo hayo yanatekelezwa katika barabara ya Morogoro kwenda Iringa na kukamilika kwake kunatarajiwa kuwaondolea kero watumiaji wa baraba hiyo.

Kaswahili amesema mfumo huo utakuwa na uwezo wa kutambua uzito wa gari likiwa kwenye mwendo usiopungua spidi 50, na kwamba mizani hiyo itakuwa na sense.

Mradi wa mfumo wa kutambua magari kabla ya kuingia kwenye mizani una lengo la kuchuja magari ambayo uzito wake haujazidi ili yaweze kuendelea na safari badala ya kuunga foleni ya kuingia kwenye mizani kwa ajili ya kupima uzito.

Meneja Kaswahili amesema mradi huo umeanza kutekelezwa Februari 2023 na utakamilika Septemba 30, 2023 na gharama zake ni Sh1.9 bilioni, kwamba kukamilika kwake kutapunguza foleni iliyopo sasa.

“Kutakuwa na sensa ambazo zitatoa kiashiria cha uzito wa gari husika na kiashiria hicho kikionyesha kuwa gari halina dalili za uzito litapita, lakini lile litakaloonyesha dalili za uzito litaingia kwa ajili ya kupima,” amesema.

Dereva lori la mafuta aliyejitambulisha kwa jina la Abiudi Rashid aliyekuwa akisafiri kwenda nchini Congo amesema changamoto zilizopo ni foleni na kuwafanya kuchelewa kufika mapema ili waweze kushusha mizigo yao na kwamba Serikali kujenga mizani hiyo ya kisasa kutasaidi kwa kiasi kikubwa kufika haraka na kuweza kurejea

Eneo la mizani ya Mikumi na Mikese ni moja ya changamoto zinazolalamikiwa na madereva wa magari hasa mabasi na malori kutokana na kuwepo kwa foleni zinazowafanya kukaa kwa muda mrefu.

Wakati huo Tanroads mkoa wa Morogoro imefanikiwa kudhibiti hatari iliyokuwa ikijitokeza katika eneo la Iyovi wilayani Kilosa barabara kuu ya Morogoro, Mikumi hadi Iringa kwa kufanya matengenezo ya kujenga kingo za mto Ruaha zilizokuwa zikisababisha barabara hiyo katika eneo la Iyovi kuwa hatarini kila mara.

Meneja Kaswahili amesema katika kudhibiti eneo hilo lililoathirika na maji ya mto Ruaha kitaalamu kiasi cha Sh480 milioni zimetumika kufanya matengenezo na kwamba lina urefu wa mita 100.

Kiasi cha Sh24 bilioni katika bajeti ya wakala wa barabara mkoa wa morogoro ya kila mwaka imekuwa ikitengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizopo chini ya wakala hao.

Jumla ya barabara zenye kilometa za barabara 271.23, yakiwemo madaraja 1,032 zimekuwa zikirejeshwa na kuimarisha miundombinu ya barabara mkoani hapa.