Mganga wa kienyeji, wenzake wawili kizimbani kwa mauaji

Mshtakiwa Ezekiel Charles (40) (Katikati) akiwa na washtakiwa wenzake, Masunga Mabula (Kulia) na Salome Raphael (kushoto) wakisubiri kusomewa shtaka la mauaji ya Ester Lukonu, mkazi wa Kijiji cha Bugumangala Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

What you need to know:

Ezekiel Charles (40), mganga wa kienyeji pamoja na wenzake wawili wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Magu kwa madai ya kumuua Ester Lukonu, mkazi wa Kijiji cha Bugumangala Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Mwanza. Ezekiel Charles (40), mganga wa kienyeji pamoja na wenzake wawili wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Magu kwa madai ya kumuua Ester Lukonu, mkazi wa Kijiji cha Bugumangala Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Wengine wanashtakiwa katika shauri hilo la mauaji namba 6/2023 ni Masunga Mabula (32) na Salome Raphael (32), ambao kwa pamoja wanadai kufanya mauaji hayo Mei 10, 2023.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali katika shauri hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Chacha Msenye ameiambia Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Amani Mahimba kuwa washtakiwa hao pia walimbaka Ester Lukoni kabla kumnyonga shingo hadi kufa.

Amedai baada ya kutekeleza mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina, washtakiwa hao walimnyofoa marehemu sehemu zake na kisha kuutelekeza mwili wake kwenye shamba la mihogo lililoko jirani.

"Washtakiwa wametenda kosa hilo la mauaji ya Esther Lukoni kinyume na Kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022," amesema Mwendesha mashtaka huyo

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo.

Hakimu Mahimba ameahirisha shauri hilo hadi Juni 16, 2023 litakapotajwa tena huku washtakiwa wakipelekwa mahabusu kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.