Mhubiri wa televisheni afungwa miaka 1,000

New Content Item (1)
Mhubiri wa televisheni afungwa miaka 1,000

Muktasari:

Mahakama ya Uturuki juzi ilimhukumu mhubiri wa dini katika televisheni kifungo cha miaka 1,000 jela kwa makosa yanayohusiana na ngono.

Istanbul, Uturuki (AFP). Mahakama ya Uturuki juzi ilimhukumu mhubiri wa dini katika televisheni kifungo cha miaka 1,000 jela kwa makosa yanayohusiana na ngono.

Mhubiri huyo, Adnan Oktar, anajulikana kutokana na tabia yake ya kupenda kutokea katika picha akiwa amezungukwa na wasichana waliovalia nguo fupi.

Oktar alikuwa akihubiri ubunifu na uhafidhina wakati wanawake waliovalia nguo zinazoonyesha, wengi wao wakiwa wamefanyiwa operesheni za kurekebisha maumbile huku wakidansi kumzunguka kufuata muziki wakati wakiwa katika studio ya televisheni.

Muhubiri huyo mwenye miaka 64 alikamatwa mwaka 2018 pamoja na watuhumiwa wengine zaidi ya 200, ikiwa ni sehemu ya msako uliofanywa na kitengo cha makosa ya fedha cha polisi jijini Istanbul.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 1,075 kwa makosa yanayojumuisha mashambulizi ya kingono, kunajisi watoto, udanganyifu na jaribio la ujasusi wa kisiasa na kijeshi, shirika binafsi la utangazaji liliripoti.

Mahakanma hiyo pia iliwahukumu watendaji wawili katika Taasisi ya Oktar, Tarkan Yavas na Oktar Babuna, kifungo cha miaka 211 na 186.

Shirika la Habari la Anadolu liliripoti kuwa Oktar pia alikutwa na hatia ya kusaidia kundi linaloongozwa na mhubiri anayeishi Marekani, Fethullah Gulen ambaye Uturuki inamuhusisha na jaribio la kupindua Serikali mwaka 2016.

Alikana kuwa na ushirikiano na Gulen na kuelezea tuhuma kuwa aliongoza kikundi cha ngono, ni uongo.

Watu 236 walishtakiwa kwa makosa hayo na 78 kati yao walikuwa wakishikiliwa mahabusu, Anadolu iliripoti. Watuhumiwa wengi wamekana kuhusika tangu walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba mwaka juzi.

Wakati wa kesi hiyo, iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu na vyombo vya habari, ilisikia taarifa za kutisha za makosa ya ngono.

Oktar alimwambia jaji Desemba kuwa alikuwa na wapenzi wapatao 1,000.

“Kuna mapenzi makubwa kwa wanawake moyoni mwangu. Penzi ni ubora wa binadamu.” alisema siku nyingine ya kusikiliza kesi hiyo Oktoba.

Oktar alianza kujulikana miaka ya 1990 wakati alipokuwa kiongozi wa kikundi kilichobainika kuwa na kashfa kadhaa za ngono.

Mwaka 2011, televisheni yake ya mtandaoni ya A9 ilianza matangazo, na kusababisha viongozi wa dini wa Uturuki wailaani.