Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miili 33 iliyoteketea ajalini Same kuagwa kesho KCMC, kukabidhiwa familia

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Miili 33 ya watu walioteketea kwa moto katika ajali ya basi wilayani Same, Kilimanjaro, itakabidhiwa kwa familia kesho Julai 3, 2025 katika Hospitali ya KCMC baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa DNA. Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 42.

Moshi. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya barabarani wilayani Same, mkoani Kilimanjaro imeongezeka na kufikia 42.

Tayari Serikali imeshatangaza kuwa kesho, Julai 3, 2025 itakabidhi miili 33 iliyoteketea kwa moto kwa familia husika baada ya kukamilika kwa vipimo vya vinasaba (DNA).

Mpaka sasa, majeruhi wawili wamebaki katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) wakipatiwa matibabu, huku wengine 24 kati ya waliokuwa wamejeruhiwa awali wakiwa wameruhusiwa.

Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini, baada ya basi la Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitoka Moshi kwenda Tanga kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitoka Same kwenda Moshi.

Baada ya kugongana, magari yote mawili yaliwaka moto, yakiwa na abiria ndani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 2, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, watu 31 waliofariki dunia walikuwa ndani ya basi dogo la Coaster (wanawake 21 na wanaume 10) na wengine 11 walikuwa kwenye basi la Chanel One,  hivyo kufanya jumla ya vifo kufikia 42.

"Mkoa umepokea na utaendelea kupokea majibu ya DNA kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Amefanya kazi nzuri na leo tumekubaliana kwamba ifikapo jioni tutakuwa tumepata taarifa kamili ya waliopimwa kupitia ndugu zao, ambao walichukuliwa sampuli za DNA Jumapili iliyopita," amesema Babu.

Amesema kesho kuanzia saa moja asubuhi, katika Hospitali ya KCMC, watakabidhi miili hiyo kwa ndugu zao ili waendelee na utaratibu wa maziko.

Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali itagharamia mazishi hayo, ikiwamo usafiri, majeneza na kutoa kiasi cha fedha kitakachosaidia kukamilisha utaratibu wote wa mazishi.

Aidha, Babu amesema miili ya watu saba, ambao wametambuliwa na ndugu zao, imeshazikwa.

"Mpaka jioni (leo), Mkemia Mkuu wa Serikali atakuwa ameshawasilisha majibu yote na kesho asubuhi, ndugu watahusika katika kutambua miili. Vilevile, viongozi wa Serikali na wa dini wataendesha ibada kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Amesema tukio la kuaga miili hiyo litakuwa la kimkoa na litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

"Jambo hili tutalifanya kwa kiwango cha kimkoa, lakini viongozi mbalimbali watafika kwa ajili ya kuaga miili kabla ya ndugu kuichukua kwa mazishi," amesema.

Kuhusu uchunguzi wa ajali, Babu amesema hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na Serikali.

"Zipo hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na Serikali pamoja na taasisi zake kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wa ajali hii na kuandaa taarifa kamili kwa vyombo vya kisheria," amesema.

Pia amesema Serikali inachunguza hali ya barabara na viashiria vya ajali, ili kuchukua hatua za kiutawala na kiufundi za kupunguza matukio kama hayo.

"Pia tutaandaa taarifa ya mwisho kuhusu tukio hili na kuwasilisha kwenye ngazi ya Taifa.

"Nawashukuru wananchi waliojitokeza kwa ushirikiano mkubwa katika tukio hili. Walishirikiana vyema na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kutoa msaada wa uokozi," amesema Babu.

Amewataka madereva na watumiaji wote wa vyombo vya usafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani, na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepuka madhara.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya ukaguzi wa magari yote ya abiria yanayoingia na kutoka stendi.

"Tumekuwa tukifanya ukaguzi wa kushtukiza na magari lazima yakaguliwe. Pia, yanapoingia stendi, kuna askari wa usalama barabarani ambao watajiridhisha kwa ukaguzi wa kila siku," amesema Kamanda Maigwa.