Mitaa Dar kujengewa barabara za lami, zege ipo ya Kwampalange
Muktasari:
- Halmashauri yasaini mikataba mitatu na makandarasi tofauti kujenga barabara kwa kiwango cha lami na zege ambazo zitakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kuondoa adha ya usafiri katika barabara za mitaa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imesaini mikataba mitatu yenye thamani ya Sh5.8 bilioni na makandarasi tofauti kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami na zege.
Katika mikataba hiyo ambayo imesainiwa na makandarasi watatu wote wanapaswa kukamilisha ujenzi huo na ndani ya kipindi cha miezi sita ambapo, barabara ya Pugu Majohe yenye urefu wa kilometa 0.4 itanufaika.
Barabara zingine ni Kitunda-Kivule, Msongola yenye urefu 0.5 kilometa, Kwampalange-Mwanagati- Kitunda urefu 0.5 kilometa zikiwa na jumla ya kilomita 1.4 kilometa zitajengwa na mkandarasi Southern Link kwa thamani ya Sh1.9 bilioni.
Kampuni ya EMJS Construction itajenga barabara ya Nyati kilometa (0.38), Rufiji kilometa (0.36) Mchikichini kilometa (0.35) zote kwa kiwango cha lami huku kiwango cha zege barabara ya Mtendeni km (0.78) na Southern kilometa (0.1) zote zikiwa na thamani ya Sh1.9 bilioni.
Wakati huo Kampuni ya Mabibo imesaini mkataba wenye thamani ya Sh650 milioni kwa ajili ya kujenga daraja la Kifuru Majoka.
Katika mkutano wa utiaji saini hizo, uliofanyika Dar es Salaam leo, Juni 2, 2023 na kushuhudiwa na vyombo vya habari makandarasi wote wamesema miradi hiyo itatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na kwa muda uliopangwa.
"Tumejipanga na tutafanya kazi kwa kuzingatia mahitaji na ubora unaotakiwa Kwa kuzingatia muda kama mkataba unavyosema," amesema Joyce Bayona, Mkadiria majenzi kutoka Kampuni ya EMJS.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo, Mhandisi Amani Mafuru amesema fedha zitakazotekeleza ujenzi huo zinatokana na asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa ndani ya halmashauri hiyo.
"Barabara zote hizo zinajengwa kutoka majimbo yote matatu Ilala, Segerea na Ukonga na zote zilikuwa na changamoto ni mategemeo yetu barabara zote zitakamilika kwa kuzingatia makubaliano ya mikataba yetu," amesema.
Kiongozi mwingine aliyehudhuria tukio hio ni meya wa Jiji hilo, Omary Kumbilamoto amesema kuna barabara nyingi ambazo zinalalamikiwa hivyo bado wataendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zingine ili zijengwe kwa zege na lami.
"Mipango imeanza na kikubwa bado tunaenda na mipango ya Serikali ya kuona barabara zote zinapitika Kwa kuzijenga Kwa kiwango cha lami na zege," amesema Kumbilamoto.