Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitandao inapomharakisha mstaafu Kinondoni!

Miaka ilee ya 1970 tulipomaliza vidato na tukajiunga na wazee wetu, kaka zetu na dada zetu kuijenga nchi hii kwa jasho na damu yetu, kitu kinachoitwa sasa “mitandao ya kijamii” kilikuwa bado kipo Sayari ya Pluto!

Hapa nyumbani tulikuwa tunategemea redio zetu za 177 na 277 za mbao tulizokuwa tukitengeneza wenyewe za National kwenye kiwanda cha waliokuwa wafadhili wa kweli, Wajapani, cha Matsushita kilichokuwa pale Barabara ya Pugu, kilichotengeneza pia redio kaseti za spika mbili, betri na feni. Hatukuwa tumeukata, lakini tulikuwa tunajitambua.

Waliotufuata kama walikuwa wanajitambua zaidi, saa hizi Matsushita yetu na vingine vingine vilivyokuwepo vingekuwa vinatengeneza TV na kompyuta za bei rahisi hapa hapa nchini, na viwanda vingekuwa kibwena, na vijana wetu wasingelazimika kuwa Gen Z wanaotafuta ajira kwa tochi!

Waulize wenzetu tuliokuwa nao, “apeche alolo”, miaka hiyo ya 60 na 70 wa Thailand na Singapore, ambao sasa wanaweza kutuuza hata kiberiti cha njiti na vijiti vya kuchokonolea meno! Halafu eti kwa nini Gen Z wetu wanaotafuta ajira kwa tochi... mchana kweupee!

Naam, “mtandao” wetu wa redio za mkulima za 177 na 277 ukafanya kazi njema ya kutuwezesha kusikiliza mpira dakika hiyo hiyo ulipokuwa ukichezwa kule “Shamba la Bibi”, Dar es Salaam, timu zetu kubwa hapa Tanzania, sio kwa Afrika, licha ya goli moja kuwezeshwa kuwa Shilingi milioni tano!

Shughuli ikawa mpira ulipomalizika, kesho yake tu Jumapili wale wa Dar es Salaam waliotaka kusoma kilichotokea, “mtandao” wetu wa magazeti ukawapa magazeti siku hiyo hiyo ya Jumapili, na watu wasome na kuangalia picha za mechi husika kefule yao.

Shughuli ikawa kwa kina sisi ambao kituo chetu cha kwanza katika kulijenga Taifa kikawa kule, mwisho wa reli Kigoma. Unaambiwa gazeti hilo la Jumapili lilipakizwa kwenye “gogo” ambalo liliingia Kigoma Jumanne, na Kigoma ile ambayo ilikuwa na kibanda kimoja tu cha magazeti pale palipokuwa sokoni.

Jumanne ile ikawa shughuli nzito ya “patashika nguo kushanika”, tukigombea magazeti ya Jumapili ili tusome na kuangalia picha za mechi ya juzi “Shamba la Bibi”. Ni miaka 40 na kitu tu iliyopita. Kumbuka, mitandao ilikuwa bado iko Sayari ya Pluto!

Ndipo “mitandao ya kijamii” hatimaye ikapiga hodi duniani na ikaingia nchini kutoka Pluto ilikokuwa. Kweli, mstaafu akauona mpira dakika ile ile ulipokuwa ukioneshwa kule ambako sasa sio Shamba la Bibi, bali kumekuwa sasa uwanja mwema na mzuri usioisha kukarabatiwa kila baada ya siku mbili tatu, sijui uonekane uzidi kuonekana mpya au watu walegeze mikanda ya suruali zao wakati sisi wengine bado tukitakiwa tuzidi kukaza mikanda! Mwe...

Kule mwisho wa reli tulikokuwa tukigombea magazeti ya Jumapili siku ya Jumanne, naambiwa sasa hata wasomaji wamepungua maana wanaangalia simu zao tu ili kujua kinachoendelea kwenye mechi za timu zao! Laiti wangejua tu kwamba miaka 40 tu iliyopita gazeti la Jumapili tulikuwa tunalipata kwa kuligombea siku ya Jumanne! Tumetoka mbali. Sio Pluto, lakini mbali!

Wanasema, “Kila chema huja na kibaya chake.” Mstaafu wetu amegundua kuwa mitandao ya kijamii inaweza pia kumharakisha kwenda Kinondoni kwa kumpa fasta habari zinazotoka “jikoni” haswa, japo hazijaiva vizuri!

Majuzi amesoma kwenye “mtandao” kuwa kibubu kinachomtunzia pensheni yake ya Shilingi laki mbili na nusu kwa mwezi, licha ya wastaafu kutaka kiongezwe na kuwa Shilingi laki tano kwa mwezi, kimetakiwa kikohoe Shilingi... mama wee!... bilioni 300 ya hela zetu ili kujenga barabara porini huko!

Mstaafu wetu hajazihakiki vyema habari hizi za mitandao yetu, lakini anahisi Kinondoni inamuita fasta kwa mshituko.  Bilioni 300! Mungu wangu...

Hela yetu wenyewe tuliyoipata kwa kukatwa mishahara yetu kwa miaka 40, na hakuna mtu hata mmoja wa angalau kutuuliza tu wenyewe! Bilioni 300 zetu! Kinondoni, hebu ngoja kwanza nifuatilie hili!


0754 340606 / 0784 340606