Prime
Mizigo inavyoibwa kwenye malori

Muktasari:
Baadhi ya vijana wamekuwa na tabia ya kupanda juu ya malori usiku na kuiba mizigo
Dar es Salaam. Ni saa saba usiku wa kuamkia Juni 23, 2025 pembezoni mwa Barabara ya Morogoro, eneo la Kwa Mfipa kuelekea Mwendapole hadi Tanita, Kibaha mkoani Pwani, linapandana kundi la vijana takribani sita wakipokezana mizigo kuishusha kutoka kwenye malori yanayofanya safari za mikoani na nje ya nchi.
Ni nyakati ambazo, isingekuwa rahisi kuona pilika pilika za watu, zaidi ya misafara na ngurumo za magari na honi. Vijana hao, hawakusubiri gari lisimame, walishusha mizigo huku gari likiendelea na safari.
Wakati hekaheka za safari za usiku kwa magari hayo zikiendelea, kundi la vijana sita waliokuwa pembezoni mwa barabara ya mchepuko (service road) nao walikuwa 'kazini.'
Vijana watatu walikuwa upande wa pili wa barabara sambamba na uelekeo wa kwenda Mlandizi na idadi kama hiyo ikiwa kwenye uelekeo wa kwenda Ubungo.
Ilipofika saa 7:48 usiku, mmoja wa vijana hao aliyekuwa upande wa uelekeo wa magari yanayokwenda Mlandizi alirukia na kuning'inia kwenye moja ya malori likiwa kwenye mwendokasi na dakika chache baadaye aliingia ndani na kuanza kurusha nje baadhi mizigo.
Wakati akifanya hivyo, vijana wengine wawili miongoni mwao wakiwa kwenye bodaboda walikuwa bize kuikusanya mizigo na kuiweka pembezoni mwa barabara.
Ilikuwa ni kazi ya kushusha na kukusanya, wakitekeleza wizi kutoka eneo la Kwa Mfipa hadi Kongowe ambako mwenzao alishuka kwa staili ambayo ni hatari zaidi ya kujiburuza kwa makalio kwenye lami wakati lori likiwa bado kwenye mwendo.
Siku ya pili, alfajiri ya kuamkia Juni 24, 2025 kazi ilikuwa ni ileile, vijana waliendelea kutekeleza kazi haramu ya wizi wa mizigo kwenye malori.
Katika kudadisi zaidi nilibaini vijana wale wengi ni wazawa wa Kibaha, wanajulikana na wengi kwa vitendo hivyo.
"Siku hizi kidogo wamepungua baada ya wengi wao kuuawa," anasema mmoja wa wenyeji wa miaka mingi wa eneo la Kwa Mfipa, Rajab Kondo (sio jina lake halisi).
Kondo anasema wizi wa mizigo kwenye malori ni kazi maarufu ya baadhi ya vijana wa eneo hilo.
"Ndio sababu hapa panajulikana kama Manzese, wezi wa hapa ni wazawa na wanajulikana, asubuhi utawaona wamekaa kijiweni ikishafika usiku kazi ni moja tu, kuiba kwenye malori," anasema Kondo.
Mbali na Kwa Mfipa, Kondo anayataja maeneo ya Mwendapole hadi Kongowe kuwa ndiyo maarufu kwa kazi hiyo.
Eneo hili ni balaa
Kauli ya Kondo haina tofauti na ya Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Salim Morcase ambaye katika mahojiano na Mwananchi anaeleza namna walivyodhibiti wizi huo.
"Kati ya Desemba, 2024 na Januari mwaka huu tuliudhibiti sana (wizi), vijana wengi walikamatwa na wengine kesi zao zinaendelea mahakamani Kibaha na Mlandizi," anasema.
Kamanda Morcase anasema 'upepo' wa wizi huo ulitulia baada ya Januari, vijana wengi waliojishughulisha na kazi hiyo haramu kukumbana na mkono wa sheria.
"Sina hakika kama wizi huo umeanza tena, Jeshi la Polisi tutafuatilia, ingawa ni kweli ulikuwepo zamani, tulishakamata kesi nyingi na watu wako mahakamini tangu Januari mwaka huu," anasema.
Anasema katika operesheni ya kutokomeza wizi huo iliyofanywa na Jeshi la Polisi, eneo korofi zaidi ilikuwa ni Mwendapole.
"Ukimaliza hicho kilima cha Mwendapole kuja jirani na Kwa Mfipa ndipo lilikuwa eneo korofi kw wizi huo, tumewakamata vijana wengi na wengi wao kama nilivyosema, kesi zipo mahakamani," anasema.
Simulizi aliyenusurika
Seif Sadick (sio jina lake halisi) ambaye alijulikana zaidi kama 'Masta' ni miongoni mwa waliowahi kuhatarisha maisha kwa kufanya kazi hiyo haramu.
Katika mahojiano na Mwananchi kwa sharti la kutopigwa picha wala kutajwa jina lake, anaeleza jinsi alivyojiingiza katika hatari hiyo.
"Hadi kutoka salama na kuachana na huo wizi ni Mungu tu," anaanza kusimulia Seif huku akieleza ambavyo vijana wengi wa eneo hilo waliokuwa kundi moja walivyopoteza maisha kwa kufanya kazi hiyo.
Anasema eneo lao la ‘kazi ya wizi’ lilikuwa ni kuanzia Kwa Mfipa kwenda hadi Kibamba na kurudi hadi Visiga.
Anasema Desemba, 2024 ndipo aliamua rasmi kuachana na maisha hayo baada ya kunusurika kuuawa kwa kupigwa nondo na utingo wa moja ya lori alilodandia kwa lengo la kuiba.
"Mara kadhaa wazazi wangu walinisihi nitoke huko, lakini sikujali, siku niliponusurika kifo na kuishi maisha ya ulemavu nilijutia, yale yalikuwa ni maisha magumu ambayo sitaki kuyarudia tena," anasimulia Seif ambaye sasa anajishughulisha na biashara ndogo ndogo.
Akieleza alivyonusurika, Seif anasema alikwenda ‘kazini’ kama kawaida na kwenye kundi lao alikuwa mtaalamu wa kudandia na kushusha mizigo hadi kupachikwa jina la Masta, siku hiyo alikutana na ajali ambayo hawezi kuisahau.
"Lilipita lori likiwa na bidhaa, kumbe utingo alikuwa amejificha nyuma akiwa na nondo, ile nimedandia alinipiga kichwani, nikadondoka, sikujua nini kiliendelea baada ya pale hadi nilipozinduka nikajikuta nipo hospitali nikiwa kwenye maumivu makali," anasema.
Anasema hadi kupona ilikuwa ni kwa nguvu za Mungu na kuanzia siku hiyo aliacha kujihusisha na wizi huo.
Hivi ndivyo unafanyika
Akieleza namna ambavyo walikuwa wakiiba, Seif anasema muda wa kazi siku zote huanza saa saba usiku hadi saa 10 alfajiri japo kuna siku unaweza kuwa chini ya hapo wakaishia saa nane au saa tisa usiku.
Anasema katika kundi wanaweza kuwa wawili hadi watatu kutegemea na ufanisi wa kazi kwa kila mmoja.
"Mkiwa wawili, mmoja jukumu lake linakuwa ni kudandia lori na kushusha mizigo na mwingine anabaki chini kwa ajili ya kuikusanya," anasema.
Seif anasema, moja ya sheria za kazi hiyo kwa hiyo kwa yule anayedandia kwenye lori lazima avae jinzi tatu hadi nne.
Anasema uvaaji huo ni kwa ajili ya kujihami wakati wa kushuka kwenye lori ili usiumie.
"Kuna staili ya kupanda na kushuka kwenye lori, kama sio mtaalamu unaweza kuumia hata kupoteza maisha," anasema Seif.
Anasema hayo yote hufanyika lori likiwa kwenye mwendo, hivyo kuna staili ya kudandia kwa visigino na kushuka kwa kuteleza kwa makalio kwenye lami.
"Huwa hakuna lori maalumu za kuiba, lolote ambalo tunaona lina mazingira rafiki ya sisi kushusha mizigo tunalidandia, kwa kuwa tuna bodaboda linapopita tunaunga nalo na mmoja kulidandia na kuanza kushusha mizigo.
"Muda wa kushusha mara nyingi huwa tunashusha bila kuchagua wala kuangalia tunashuha nini hasa kwa bidhaa ambazo zimefungwa, tunazikagua baada ya kumaliza kazi," anasema.
Katika ukaguzi wa mizigo, Seif anaeleza kuna siku wenzao katika kazi waliwahi kushusha viroba vya mbolea wakidhani ni sukari.
"Walivishusha kwa fujo, baada ya kazi ile kuangalia ni mbolea, wakaziacha pale pale barabarani," anasema.
Kwa mujibu wa Seif, wanapofanikiwa kuiba, uhifadhi bidhaa eneo moja na kutafuta wateja.
"Hii kazi haina wateja maalumu, japo wapi baadhi hujirudia rudia kutokana na kutotuumiza kwenye bei.
"Hata hivyo tunapokuwa na bidhaa, tunaangalia tuipeleke wapi ambako itauzika kwa urahisi," anasema.
Hatari ya kazi
Seif anasema kuiba mizigo kwenye malori ni kazi hatari kwa kuwa, kwao ilikuwa kupata ulemavu au kuuwa ni kitu cha kawaida.
Anasema wenzao kadhaa wamepoteza maisha na wengine kupoteza viungo vya mwili kutokana na kazi hiyo.
"Hapa Kwa Mfipa hadi Mwendapole likuwa ni mtandao mkubwa, wengi wameuawa, kidogo hali ikapoa, lakini ndiyo chanzo cha kuitwa Manzese," anasema.
Seif anaeleza mmoja wa washirika wake alivyopoteza mkono wa kulia kwa staili hiyo hiyo baada ya kukatwa na panga akiwa anadandia lori ili kuiba.
"Matukio ya kupigwa tumekutana nayo sana, wapo waliopoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa maisha, inaumiza," anasema.
Wasemacho madereva
Baadhi ya madereva wa malori wanaeleza namna ambavyo wezi hao wamekuwa wakiwapa hasara.
"Kuna siku niliwahi kulipishwa mzigo nilioibiwa pale Mwendapole, roho iliniuma nikasema nitalikomesha hili mimi mwenyewe na nilifanya hivyo," anasema dereva wa lori linalofanya safari kwenda Tunduma hadi Zambia," Kapalatu Joseph.
Dereva mwingine, Nelson Elisha anasema kutoka Kibamba hadi kufika Mlandizi dereva akipita eneo hilo salama bila kuibiwa anashukuru.
"Ilifikia hatua tukawa tunatumia mbinu ya kuweka miba nyuma ya lori ili wezi washindwe kudandia, pia kujibanza kuwapiga, lakini hii inahitaji moyo wa ujasiri, ikiwezekana polisi iimarishe doria kwenye maeneo hayo usiku," anasema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo (Tamstoa), Chuki Shabani ameiambia Mwananchi kuwa changamoto ya wizi huo inaathiri kibiashara.
"Hilo tatizo lipo sana Barabara ya Morogoro, mizigo ya watu inaibwa, kuna nyakati tuliwahi kukaa vikao na Wizara ya Ujenzi kuomba watusaidie hiyo barabara ipanuliwe hadi Morogoro, labda itapunguza changamoto, lakini bado michakato haijafanikiwa," anasema.
Pia, anasema wizi huo unawaathiri mara kwa mara kutokana na mizigo kufika ikiwa imepungua.
“Wenye malori hulazimishwa kulipa ile iliyoibwa, jmbo ambalo linawarudisha nyuma kama wafanyabiashara,”anasema Shaban.
MWISHO