Mjukuu atuhumiwa kumuua bibi yake kwa panga

Majirani wakiwa nyumbani wa Bibi Agness Karoli anayedaiwa kuuawa  na mjukuu wake.  Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Tukio hilo linadaiwa kutokea Aprili 6, 2024 ambapo bibi huyo, Agnes Karoli (70) alichomwa na kitu chenye ncha kali na mjukuu wake, Wahaki Mashaka (28) akiwa nyumbani kwake.

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Wahaki Mashaka (28) kwa tuhuma za kumuua bibi yake, Agnes Karoli (70) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali.

Kifo cha bibi huyo kinadaiwa kutokana na kuvuja damu nyingi kwenye majeraha aliyochomwa mapanga na mjukuu wake.

Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 7, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema lilitokea Aprili 6,2024 ambapo bibi huyo alichomwa na kitu chenye ncha kali baada ya kuvamiwa na mjukuu wake akiwa nyumbani kwake.

“Bibi huyo akiwa nyumbani kwake, ghafla alivamiwa na mjukuu wake ambaye alikuwa na panga, akaanza kumshambulia kwa kumkatakata na kumuua kabla majirani hawajafika eneo hilo na kumkamata na baadaye taarifa hizo zilifika Polisi. Tulifika haraka na kumuokoa mtuhumiwa (Wahaki) kutoka kwenye mikono ya wananchi waliotaka kumuua.”

“Kwa sasa tunaendelea na jitihada za upelelezi kuhusiana na tukio hilo ili mtuhumiwa aweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria ambapo katika kushambuliwa na wananchi alipata majeraha machache, lakini kwa yuko mikononi mwetu,” amesema Mkama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama

Akizungumzia mkasa huo, mtoto wa marehemu na mama mzazi wa mtuhumiwa, Mwanahamisi Omary amesema aliyefariki ni mama yake mzazi Aprili 6, 2024 saa 8 mchana walipomaliza kula chakula cha mchana, yeye na watoto wake pamoja na mama yake waliagana kwamba wanakwenda msibani.

Amesema baada ya mama yake kusikia naye anakwenda kwenye msiba huohuo, alimwambia atapumzika ili aende (Mwanahamisi), aliondoka na kwenda msibani.

“Wakati niko msibani, nikaambiwa kuwa mdogo wangu na mtoto wangu wananitafuta, nikauliza kwa nini wananitafuta, nikaambiwa hawajui wale majirani sasa, ikabidi nirudi nyumbani haraka, nilipofika nikafungua mlango nikakuta mama amelala chini na damu nyingi zinamwagika,” amesimulia.

Mwanahamisi amesema hakujua aliyefanya tukio hilo, akaanza kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani, baada ya muda mfupi watu wakajaa na mtoto wake akawa anasema haelewi aliyetekeleza mauaji hayo.

“Mwanangu akaondoka, wananchi wakaanza kumfuatilia, wakamkuta mwanangu Wahaki akiwa msikitini anaswali, yeye mwenyewe anashangaa hili tukio, akawa analia tu. Baada ya hapo akakamatwa, akapelekwa Polisi akituhumiwa kwamba yeye ndiye anadaiwa kumuua bibi yake,” amesema Mwanahamisi.

Hata hivyo Mwanahamisi amesema mtoto wake Wahaki Athuman Mashaka ndiye anatiliwa shaka kuhusika na tukio hilo kwa kuwa alikua hayuko vizuri kiakili.

“Baada ya kutokea kwa lile tukio, majirani wakaanza kusema mtoto wangu ndiye kahusika kutokana na kwamba alikua ana matatizo ya akili kwa muda mrefu kidogo, ndiyo maana lilivyotokea wakamuhisi kwamba yeye ndiye amesababisha mauaji haya ndio wakamkamata,”amesema Mwanahamisi.

Kwa upande wake Zaituni Athuman Mashaka, mjukuu wa marehemu na dada wa mtuhumiwa amesema kaka yake alikuwa na matatizo ya akili

“Kaka yangu alikua na matatizo ya akili yaliyomuanza kwa muda kidogo wakati akiwa Dar es salaam na hata aliporudi hapa nyumbani ndio akaanza kuchanganyikiwa kabisa maana kuna wakati tunaweza kuwa tunaongea kama ndugu ghafla anaanza kupiga kelele, wakati mwingine analia, tukiuliza vipi hasemi lolote anabakia analia tu.”

“Siku nyingine tulitoka nyumbani, akabaki yeye, akachukua nguo zake na zetu akaanza kuzichoma moto, akahamia upande wa baba anapoishi, nako akazichoma moto, kuhusu tukio la jana nilikua kazini, nikaambiwa twende nyumbani, nahitajika.

“Nilipofika nyumbani nikakuta watu wengi, nikauliza kuna nini, wakaniambia niende tu, nilipofungua mlango nikakuta bibi kafariki na pembeni yake kulikua na panga, baada ya kuona hivyo, nikaanza kulia,” amesema Zaituni.

Baba mdogo wa mtuhumiwa huyo, Pius Clemence, amesema kwa taarifa alizokuwa nazo kuhusu mtoto wake huyo, ni kwamba alishachanganyikiwa na akawa mtoto wa kuweweseka.

“Nilijaribu kumchukua kidogo nikampeleka sehemu ili apate matibabu, alipewa matibabu kama baada ya mwezi mmoja hivi, baadaye hali yake ikabadilika, akaanza kuchoma magodoro nyumbani kwao, akachoma la mama yake, akachoma na la baba yake, baadaye akaja kwangu kutaka kuchoma, akapiga hodi nilikuwepo nilipotaka kufungua akakimbia.

“Baada ya hapo, akaenda Dar es Salaam kisha akarudi hapa Morogoro, hadi anafanya hili tukio hajamaliza hata wiki tangu atoke Dar es Salaam maana kama siku mbili nyuma alikua ametoka kuchoma moto nguo za huyo bibi yake,” amesimulia Clement.

Rafiki wa marehemu, Salum Khamisi amesema alikuwa akiishi vizuri na Wahaki lakini kwa siku za karibuni alibadilika na kuanza kuchanganyikiwa, baada ya kuanza kutumia dawa ya kulevya ambazo zilimzidi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji cha Changarawe kilichopo wilayani Mvomero, Fred Matagaru amesema taarifa za kifo hicho aliipata baada ya kupigiwa simu na mwananchi wake.

“Jana  saa 9 alasiri nilipigiwa simu na mwananchi kwamba nifike hapa bibi Agnes amekufa kwa kupigwa panga na mjukuu wake. Nilifika hapa  lengo kujiridhisha, niliingia ndani nikakuta kweli, kuna damu zimetapakaa, kuna panga na kisu mle ndani. Baadaye nilitoa taarifa Polisi nao walifika kwa wakati, wakachukua vipimo, maelezo kwa familia na viongozi wa kijiji hiki.”