Mke adaiwa kumuua mumewe kwa kumpiga na rungu kichwani

Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga akitoa pole kwenye msiba wa mume ambaye anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na rungu kichwani

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoani Iringa linamshikilia Aurelia Kalolo (40) akituhumiwa kumuua mume wake, Williad Ngamema kwa kumpiga na rungu kichwani katika kijiji cha Ukumbi wilayani Kilolo.

Iringa. Mkazi wa Kijiji cha Ukumbi, wilayani Kilolo, Aurelia Kalolo (40) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa akituhumiwa kumuua mume wake, Williad Ngamema kwa kumpiga na rungu kichwani.

Akisimulia tukio hilo, Mtendaji wa Kijiji cha Ukumbi, Mariam Kaduma amesema alipata taatifa za mauaji hayo siku mbili zilizopita, saa tisa usiku.

Amesema alipofika nyumbani kwa wanandoa hao alikuta mume ameshauawa na hivyo kupiga simu polisi huku akimshikilia mtuhumiwa huyo.

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema wanandoa hao walikuwa na ugomvi tangu asubuhi.

"Jioni mwanamke alitaka kumpiga mume wake na rungu tukasuluhisha, akaondoka na kwenda kirabuni kunywa pombe kumbe usiku aliporudi akachukua tena rungu na kumpiga mume wake ambaye amefariki," amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema upelelezi juu ya tukio hilo unaendelea.

Akizungumza kwenye msiba huo, Nyamoga amesema chuki, hasira na visasi ndani ya ndoa vimekuwa vichocheo vya ukatili na mauaji kama ilivyotokea kwa familia hiyo.

"Inaumiza na kusikitisha, hali hii ni hatari kwa sababu familia ambayo ilipaswa kuwa mahali salama yanatokea mauaji, tuzungumze, tushirikishe wazee,viongozi wa dini na watu wenye hekima tukiwa na migogoro ya familia, kupigana na kuuana sio sawa," amesema Nyamoga.