Mke asimulia alivyokatwa titi, mkono na mumewe Rorya

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, limesema linamtafuta mkazi wa kijiji cha Isango kata ya Nyamunga wilayani Rorya, Werema Ibaso anayedaiwa kumkata titi na mkono mkewe, Maria Marwa (36) kutokana na wivu wa mapenzi.

Musoma. Mkazi wa kijji cha Isango wilaya ya Rorya, Maria Marwa (36) amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mara baada ya kudaiwa kukatwa mkono na titi na mumewe.

Mwanamke huyo alipata majeraha hayo baada ya kuibuka ugomvi baina yake na mume wake huku chanzo kikidaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo mbali na kukatika mkono na titi, amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akizungumza na Mwananchi akiwa hospitalini leo Jumanne, Septemba 20, 2022, Maria amesema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 7 saa 3 usiku.

Amesema kuwa siku ya tukio baada ya kupata chakula cha usiku waliingia ndani kulala kama kawaida lakini ghafla mume wake, Werema Ibaso alimtaka akambidhi simu yake na kutii.

Ameeleza kuwa baada ya kumkabidhi alimrudishia na kumuambia aanze kupitia majina kwenye simu hiyo huku akimuuliza namba ya mtu aliyempigia siku mbili zilizopita.

"Alinirudishia simu na kunitaka nianze kupekua majina ya kwenye simu nilipekua majina yote akataka nipekue tena mara ya pili nilipomaliza akaniuliza namba ya mtu aliyenipigia juzi yake nikamwambia mimi huyo mtu simjui" amesema

Amesema kuwa baada ya kukosekana kwa namba ya huyo mtu, mume wake alichukua panga kutoka kwenye uvungu wa kitanda na kuanza kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili wake na kabla ya mtoto wao kukimbilia kwa majirani kuomba msaada.

 Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto sita amesema kuwa baada ya majirani kupata taarifa na kufika eneo la tukio mume wake alifungua mlango na kuwatishia kwa panga kisha kutoroka kusikojulikana.

Akimzungumzia mgonjwa huyo, Daktari wa hospitali hiyo, Nurdin Nuru amesema kuwa walilazimika kumkata mkono mwanamke huyo baada ya kufika hospitalini hapo akiwa tayari mkono umeharibika.

"Tulimpokea hapa Septemba 8 mkono ukiwa tayari umeharibika huku titi la kushoto likiwa limening'ing'inia na mkono uliharibika kwasababu panga lililotumika lilikuwa chafu,

Mpaka anafika mkono ulikuwa una usaha na tayari ulikuwa umeanza kuharibika" amesema

Dk Nuru amesema kuwa mwanamke huyo alifika hospitalini hapo pia akiwa na majeraha ya panga kisogoni, ubavuni, shingoni na kwamba hivi sasa anaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Geofrey Sarakikya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Sarakikya amesema jeshi la polisi linaendelea kumsaka mwanaume huyo aliyetoroka baada ya kufanya tukio hilo.