Prime
Mke wa mvuvi aliyeuawa kisa Sh1,000 asimulia maneno ya mwisho ya mumewe
Muktasari:
- Familia ya Salim Hussein, mvuvi aliyepoteza maisha baada ya kuchomwa kisu na rafiki yake wa karibu Aprili 27, 2026 kwa madai ya deni la Sh1,000, bado iko kwenye majonzi makubwa huku mke wake akisimulia maisha yao.
Tanga. “Mke wangu, umwangalie mtoto wetu.” Hayo ni maneno ya mwisho ya Salim Hussein, mvuvi aliyeuawa na rafiki yake kisa deni la Sh1,000 alilokuwa akidaiwa, jambo ambalo limeibua simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Mke wa marehemu, Aisha Omari anasimulia maisha yao na maneno ya mwisho aliyoambiwa na mume wake kabla hajakutana na umauti, tukio ambalo limeacha majeraha kwa familia, ndugu na jamii iliyoshuhudia mwisho wa maisha ya kijana huyo aliyekuwa tegemeo la familia yake.
Aisha, mama wa mtoto mmoja aliyezaa na marehemu, anasema maisha yao yalikuwa ya furaha na matumaini makubwa kabla ya kifo chake.
Anaeleza kuwa hakuwahi kufikiria kwamba siku moja angempoteza mumewe katika mazingira ya kusikitisha kiasi hicho. Kwa sasa anasema bado ana maumivu makubwa na haamini kilichotokea.
“Nilikuwa naamini tutazeeka pamoja. Sikuwahi kuwaza kwamba siku moja ningemuona amelala chini bila uhai huku watu wakimzunguka kwa huzuni,” anasema Aisha huku akifuta machozi.
Anasema picha ya siku hiyo bado haijafutika kichwani mwake na kila anapokumbuka hujikuta akilia tena. Maumivu ya kumpoteza mwenza wake bado yanaendelea kumtesa kila siku.
Walivyoanza maisha
Aisha anasema safari ya mapenzi yao ilianza kwa namna ya kawaida baada ya marehemu kumuita alipokuwa akipita njiani kuelekea kwenye shughuli zake za kila siku.
Mazungumzo yao yakaanza taratibu hadi baadaye wakajikuta wameingia kwenye uhusiano wa dhati uliokuwa umejaa upendo. Kadri siku zilivyokwenda ndivyo walivyozidi kuaminiana na kupanga maisha yao ya baadaye.
“Baada ya kuelewana, aliamua kunipeleka kwake na siku hiyo tukaanza maisha pamoja. Aliniambia alikuwa na ndoto ya kuwa na familia na mtoto, ndipo tukaanza kupanga maisha yetu huku tukijiandaa kufunga ndoa rasmi,” anasimulia.
Aisha anasema walikuwa na mipango mingi ya maendeleo ambayo waliamini ingeweza kutimia kupitia ushirikiano wao. Hakuna aliyedhani ndoto hizo zingekatishwa ghafla namna hiyo.
Baadaye walienda Wilaya ya Pangani ambako baba mzazi wa marehemu anaishi. Anasema Salim alikuwa mtu mwenye upendo mkubwa kwa familia yake na hakupenda kabisa migogoro au ugomvi na watu wengine.
Anaeleza kuwa marehemu alikuwa mtu wa watu na kila aliyekuwa karibu naye alimkubali kutokana na tabia yake nzuri.
“Alikuwa mtu mpole sana. Hakuwahi kugombana ovyo na kila siku alikuwa akifikiria familia yake kwanza,” anasimulia kwa sauti ya huzuni.
Aisha anasema jambo hilo ndilo linalomuumiza zaidi kwa sababu hakutegemea mtu mwenye tabia ya upole angeweza kufa kwa namna ya kikatili kiasi hicho. Anaamini bado familia yao ilikuwa inamhitaji sana.
Kwa mujibu wa Aisha, shughuli kuu ya mumewe ilikuwa ni uvuvi ambao ulimwezesha kuhudumia familia yao. Anasema kazi hiyo ndiyo iliyokuwa tegemeo lao kuu kwa chakula, kodi na mahitaji mengine muhimu ya nyumbani. Kupitia kazi hiyo waliweza kuendesha maisha yao ya kila siku bila matatizo makubwa.
“Kazi ya uvuvi ndiyo iliyokuwa inatuweka mjini. Kila siku akienda baharini alikuwa anarudi na samaki kwa ajili ya familia yake. Alihakikisha mtoto wake anapata kila kitu muhimu,” anasema.
Anaongeza kuwa marehemu alikuwa akijituma kuhakikisha familia yake haikosi mahitaji muhimu hata kama kipato kilikuwa kidogo.
Kuhusu rafiki aliyemchoma kisu mumewe, Aisha anasema alikuwa akimsikia kama rafiki wa marehemu huko baharini lakini hakuwahi kumuona nyumbani kwao.
Anasema alimfahamu vizuri baada ya tukio hilo kutokea na kuonyeshwa picha zake na baadhi ya watu waliokuwa karibu na marehemu. Hali hiyo ilimshangaza kwa sababu hakuwahi kuhisi kuna tatizo lolote kati yao.
“Sikuwahi kujua kama walikuwa na tofauti yoyote. Nilikuwa najua ni marafiki wa kawaida tu,” anasema. Anaeleza kuwa mpaka leo bado anajiuliza ni nini hasa kilichoweza kumfanya mtu aliyekuwa rafiki wa karibu kuamua kuondoa uhai wa mwenzake kwa sababu ndogo kiasi hicho.
Siku ya mwisho ya mumewe
Akizungumzia mazungumzo yao ya mwisho na marehemu mume wake, Aisha anaanza kulia, machozi yanamzidi na kushindwa kujizuia mbele ya watu waliokuwa wakimsikiliza.
Anakumbuka kila tukio la siku hiyo kana kwamba limetokea muda mfupi uliopita. Maumivu ya maneno ya mwisho ya mumewe bado yanamtesa kila anapokumbuka.
“Kabla hajaondoka kwenda baharini, nilikuwa tayari nimempikia chakula na nikamwekea kwenye bakuli ili ale akiwa huko.
“Alipokuwa anatoka aliniambia, ‘Mke wangu, umwangalie mtoto.’ Wakati huo mtoto wetu alikuwa ana homa. Ilikuwa saa 11 alfajiri,” anasema. Kauli hiyo imeendelea kubaki moyoni mwake kama kumbukumbu ya mwisho kutoka kwa mumewe.
Baada ya maneno hayo, Aisha anasema hakuwahi tena kuwasiliana na mumewe mpaka alipopata taarifa kwamba amechomwa kisu na kufariki dunia.
Anasema taarifa hiyo ilimchanganya kwa sababu muda mfupi kabla ya hapo walikuwa wamezungumza kawaida kabisa. Hakuwahi kufikiria kwamba huo ungekuwa mwisho wa mawasiliano yao duniani.
Anasema taarifa hizo alizipokea kutoka kwa wapita njia wakati akiwa njiani kumpeleka mtoto wao hospitalini kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Mtoto alikuwa hajalala vizuri usiku kucha kutokana na homa kali. Hata hivyo, safari hiyo ya hospitali iligeuka kuwa safari ya majonzi baada ya kupata taarifa za msiba.
“Nilipoambiwa nilizimia palepale. Baada ya kuzinduka ndipo nikaenda eneo la tukio na kumkuta tayari amefunikwa huku watu wakisubiri polisi wafike,” anasema.
Aisha anasema wakati huo alikuwa haamini kilichokuwa kimetokea hadi alipofika eneo la tukio na kuuona mwili wa mumewe ukiwa chini.
Aisha anaiomba Serikali kuhakikisha mtuhumiwa anachukuliwa hatua kali za kisheria ili tukio hilo liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kutumia vurugu kutatua migogoro.
Anaamini haki ikitendeka itasaidia kupunguza matukio ya aina hiyo katika jamii. Pia bado haamini kama mtu anaweza kuondoa uhai wa mwenzake kwa sababu ya fedha kidogo kiasi hicho.
“Ninachoomba ni sheria ichukue mkondo wake. Haiwezekani mtu auawe kwa sababu ya Sh1,000,” anasema.
Maisha baada ya kifo
Aisha anasema maisha yake yamebadilika tangu kifo cha mumewe. Anaeleza kuwa changamoto kubwa anayopitia sasa ni ugumu wa maisha pamoja na jukumu zito la kulea mtoto wao akiwa peke yake bila msaada wa mwenza wake.
Kila siku anawaza namna atakavyoweza kuendesha maisha katika mazingira hayo magumu.
“Mlipaji alikuwa yeye. Sasa sijui nifanye nini. Kodi ya nyumba inakaribia lakini sina hata pa kuanzia,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa analazimika kuwa mama na baba kwa mtoto wake huku akipambana kutafuta namna ya kuendelea kuishi.
Anasema hadi sasa hajapata msaada wowote kutoka kwa ndugu, jamaa wala marafiki, lakini anajitahidi kubaki imara kwa ajili ya mtoto wake ambaye sasa anamtegemea yeye.