Mkunga Mtanzania atunukiwa nishani ya heshima Canada
Muktasari:
Zawadi hiyo imetolewa na shirika lisilo la kiserikali linalotetea haki za watoto la Save the Children na shirikisho la kimataifa la wakunga wakati wa mkutano wao uliofanyika Toronto nchini Canada hivi karibuni.
Dar es Salaam. Mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Ukunga na Uuguzi cha Aga Khan, Loveluck Mwasha pamoja na Raia wa Afghanistan, Amina Sultani wametunikiwa zawadi ya heshima ya ukunga ya mwaka 2017.
Zawadi hiyo imetolewa na shirika lisilo la kiserikali linalotetea haki za watoto la Save the Children na shirikisho la kimataifa la wakunga wakati wa mkutano wao uliofanyika Toronto nchini Canada hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Joe Lugalla amesema jana (Ijumaa) kuwa wakunga hao wamepewa zawadi kwa utumishi uliotukuka katika kuendeleza fani ya ukunga katika nchi zao licha ya changamoto zilizopo.
Amesema tukio hilo lilihudhuriwa na Rais wa Jumuiya ya Wakunga, Frances Day-Stirk na Ofisa Mtendaji Mkuu Save the Children Patricia Erb.
“Mwasha amefanya kazi ya ukunga kwa miaka 30 pia ni balozi wa fani hiyo akipigania kuboreshwa kwa mazingira ya kazi pamoja na afya ya mama na mtoto wakati wa kujifungua nchini hapa nchini,” amesema Profesa Lugalla.
Amesema mbali na hilo, Mwasha Pia amekuwa akitoa ushauri kwa wakunga mbalimbali kupitia mabaraza ya wakunga na pia katika chuo hicho na Hospitali ya Aga Khan.
Akipokea zawadi hiyo, Mwasha ametaja siri ya mafanikio yake kuwa ni kufanya kazi kwa bidii na kupenda taaluma yake.
“Kazi yangu imenipa pia fusra ya kupigania upatikanaji wa vetendea kazi wezeshi na mafunzo stahiki kwa wataalamu wote wa fani hii,” amesema
Ameongeza; “Wanafanya kazi kwa ukaribu na wadau mbalimbali kama njia mojawapo ya kutambua mchango wa wakunga katika jamii.”