Mkurugenzi, mkewe wafa maji Mpwapwa

Muktasari:

Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa mifugo kanda ya kati, Dk Harun Chawala na mkewe, Neema Mwasanganga  wamefariki  baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa maji wakati wakivuka daraja la Shaaban Robert mjini Mpwapwa.

Mpwapwa. Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa mifugo kanda ya kati, Dk Harun Chawala na mkewe, Neema Mwasanganga  wamefariki  baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa NA maji wakati wakivuka daraja la Shaaban Robert mjini Mpwapwa, Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti Tanzania, Dk Jonas Kizima amesema leo Jumamosi Machi 6, 2021 kuwa tukio hilo limewasikitisha kutokana na kupoteza nguvu kazi ya Taifa na taasisi ya utafiti Tanzania.

Amesema Dk Chawala alikuwa anampeleka mkewe kazini kwenye hospitali ya wilaya, lakini walipo fika kwenye daraja hilo maji yaliwazidi na kusombwa.

Dk Kizima amesema tukio hilo limetokea jana saa 2  usiku baada ta gari hilo aina ya Nissan lenye namba za usajili T483 BRR kusombwa na maji kwenye daraja hilo lililopo mita chache kutoka ilipo ofisi ya mkuu wa wilaya.

Kutoka gari ilipotumbukia hadi ilikokutwa miili ni umbali wa karibu kilomita 18 na ilikuwa katika maeneo tofauti .

Mashuhuda wanasema mwili wa mwanamke ulikutwa kitongoji cha Kwamshango  kilomita 15 kutoka walipotumbukia wakati mwili wa Dk Chawala ulikutwa kitongoji cha Isinghu umbali wa  kilomita 18.

Miili yote imepatikana imehifadhiwa katika hospitali ya Mpwapwa ikisubiri taratibu za ndugu na Serikali.

imeandikwa na Lwitiko Mwamakula