Mnzava: Shughuli za kibinadamu zinaathiri upatikanaji wa maji
Muktasari:
- Mradi wa Itagano-Mwasekwa umewekewa jiwe la msingi leo Jumapili Agosti 25, 2024 na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava huku kwa Mkoa wa Mbeya ukitarajia kuzindua miradi 56 yenye thamani ya Sh39.8 bilioni.
Mbeya. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji, kwani huviathiri.
Pia aliwataka wananchi kuvitunza ili kuisaidia Serikali kutotumia gharama kubwa kuvirejesha.
Mnzava ameyasema hayo leo Jumapili, Agosti 25, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Itagano - Mwasekwa unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya -Uwsa) wenye thamani ya Sh5 bilioni, unaozalisha maji lita milioni mbili kwa siku.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza miundombinu ya maji maeneo ambayo kuna vyanzo vya uhakika na kuwataka wananchi kuvitunza vilivyopo, kwa kuachana na shughuli za kijamii ili wapate huduma safi na salama ya uhakika.
"Wananchi tunzeni vyanzo vya maji mkiendeleza shughuli za kijamii, vinaweza kukauka na kusababisha ukosefu wa huduma hiyo muhimu, kwani Serikali ya awamu ya sita imeweka mikakati kuhakikisha mnapata maji safi na salama maeneo ya karibu," amesema.
Mnzava amesema Serikali imeanza kutekeleza mradi wa Itagano - Mwasekwa lengo ni kuona jamii inafurahia huduma ya maji safi na salama, sambamba na kutoa maelekezo ya kutekelezwa haraka na Mbeya-Uwsa ifikapo Desemba mwaka huu.
"Tumeona miundombinu iliyowekwa sambamba na tenki la kutibu maji ni mradi mkubwa ambao Serikali itaendelea kuleta fedha nyingi, lengo ni kuona wananchi wanapata huduma bora za maji safi na salama," amesema.
Amesema wamepitia nyaraka za utekelezaji wa mradi huo na kuridhishwa, kikubwa ni kuona maelekezo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mbeya (Mbeya -Uwsa), Mhandisi Gilbert Kayange amesema utekelezaji wa mradi wa Itagano - Mwasekwa utaongeza uzalishaji wa maji lita milioni mbili kwa siku.
Amesema ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa, mamlaka wanaendelea kusaka vyanzo vingine vya maji. “ Mahitaji ya maji kwa sasa ni lita milioni 90 huku uzalishaji ni lita milioni 71 kwa siku,”amesema.
Naye Mbunge viti Maalumu Wanawake Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amesema wana kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa kuleta miradi ya kimkakati.
"Mradi huu wa Itagano - Mwansekwa unakwenda kuwa mwarobaini na kumtua mama ndoo kichwani, sambamba na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miradi ya maendeleo hususan katika sekta ya afya,” amesema Fyandomo.
Naye mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Iganzo Kata ya Igodima jijini hapa, Sophia Mpama amesema awali kabla ya ujio wa mradi huo wananchi walikuwa wakitumia maji ya visima na mito, hivyo watautunza mradi huo na mingine.