Morogoro watakiwa kulinda miundombinu ya umeme

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akizungumza na wananchi wa kijiji Cha Maseyu kata ya Gwata Wilaya ya Morogoro ambapo umeme katika kijiji hicho tangu kuanzishwa kwake Mwaka 1974 hakijawai fikiwa na umeme. Lilian Lucas

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema ifikapo Juni 2024 vijiji vyote nchini na baadhi ya vitongoji vitakuwa tayari vimeunganishwa na umeme kupitia REA.

Morogoro. Naibu Wizara wa Nishati, Judith Kapinga amewataka wananchi katika kijiji cha Maseyu Wilaya ya Morogoro kuendelea kulinda miundombinu ya umeme inayojengwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili wapate maendeleo.

Aidha Naibu Waziri huyo amesema ifikapo Juni 2024 vijiji vyote nchini na baadhi ya vitongoji vitakuwa tayari vimeunganishwa na umeme kupitia REA.

Naibu Waziri Kapinga amesema hayo Novemba 29, 2023 wakati akiwasha umeme katika Vijiji vya Maseyu na New Land vilivyopo katika Halmshauri ya wilaya ya Morogoro ikiwa uzinduzi rasmi wa umeme wa mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

"Hivi Sasa umeme sio tena anasa bali ni huduma kwa kila mwananchi kwaajili ya kuleta maendeleo hivyo tutahakikisha ifikapo June 2024 vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme'amesema Naibu Waziri huyo wa Nishati.

Aidha Kapinga amewaagiza wakandarasi wote nchini wanaojenga miradi ya umeme ikiwemo ile ya REA (miundombinu) kuhakikisha miradi hiyo wanakamilika kwa wakati.

Amesema Serikali ya sasa sio ya maneno wala ya makaratasi bali ya vitendo ndio maana inafanya kazi kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Nia ya Serikali ni kuona vijiji vyote hapa nchini vinawaka kwa kuwa bila nishati hakuna maendeleo hivyo tunaomba wananchi mtusaidie kulinda miundombinu ya umeme kwakuwa inagharimu fedha nyingi," amesema Naibu Waziri huyo.

Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema Morogoro ina jumla ya vijiji 699 kati yake vijiji 412 vina umeme na vijiji 257 vilikuwa havina umeme na kupitia mradi wa REA tayari vijiji 177 vimeshaunganishwa na umeme na vilivyobaki vipo katika hatua za mwisho kumalizia.

Amesema mradi wa REA kwa vijiji vyote katika mkoa wa Morogoro unagharimu jumla ya Sh78.1 bilioni na tayari katika Halmshauri ya Wilaya ya Morogoro, Vijiji 87 vimeshapatiwa umeme.

Naye Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu kwa jin la Babu Tale, ameiomba Serikali kufikisha umeme kwenye migodi ya kuchimba madini ikiwemo dhahabu ili kuchochea ajira na kukuza uchumi.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kufanya uchimbaji kutokana na kukosa huduma hiyo.