Moto wenye utata

Moto wenye utata

Muktasari:

  • Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiunda kamati ya kuchunguza tukio la moto ulioteketeza maduka na mali za wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo, maswali lukuki yameibuka kuhusu janga hilo.


Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiunda kamati ya kuchunguza tukio la moto ulioteketeza maduka na mali za wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo, maswali lukuki yameibuka kuhusu janga hilo.

Miongoni mwa maswali ambayo yamezua utata ni pamoja na muda wa moto huo kuanza, sababu za Zimamoto kukosa maji eneo la Kariakoo na makao makuu ya kikosi hicho, yaliyoko Upanga, takriban kilometa moja kutoka sokoni hapo.

Moto huo ambao kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ulianza juzi saa 2:30 usiku, umeteketeza eneo la juu la soko hilo lililokuwa limesheheni maduka mbalimbali yakiwamo ya dawa za mifugo, mabucha ya nyama na samaki, mawakala wa pesa na ATM za benki.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa moto huo ulianza majira ya saa 1: 40.

Akizungumza jana baada ya kukagua eneo la tukio, Waziri Mkuu Majaliwa alitangaza kuipa siku saba za awali kamati aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto katika soko hilo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo.

Alisema kamati iliyoundwa itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-Tamisema na ofisi ya Waziri Mkuu itakayowakilishwa na mkurugenzi wa maafa.

Wengine ni vyombo vya ulinzi na usalama vikijumuisha Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Zimamoto pamoja na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Pia, Waziri Mkuu alizitaja taasisi nyingine kuwa ni Wakala wa Majengo, Shirika la Umeme (Tanesco), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

“Endapo itagundulika kuna mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike moto,” alihoji Majaliwa.

Kiongozi mwingine aliyefika sokoni hapo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Ummy Mwalimu ambaye alitembelea eneo hilo na kutaja idadi ya wafanyabiashara walioounguliwa mali zao kufikia 224.

Ummy aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunga miundombinu itakayoweza kusaidia pindi ajali kama hizo zinapotokea, katika masoko yote.

Chanzo cha moto

Kuna maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuhusu chanzo cha moto huo ambao umeathiri mitaji ya wafanyabiashara.

Wakati Serikali ikiendelea na uchunguzi wake, baadhi ya wafanyabiashara walisema awali walisikia mlio mkubwa mithili ya bomu, kisha wakaanza kuona moshi ukitoka, ndipo walipoanza kuomba msaada.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Ibrahim Katera alisema moto huo ulianza saa 1:40 na baadaye gari moja la Zimamoto lililofika awali lilishindwa kuuzima moto na la pili pia halikuweza na kusababisha usambae zaidi.

“Nilianza kushirikiana na mwenzangu kuanza kuzima moto huo lakini wakati huo ulikuwa umeshakuwa mkubwa, vitu vyetu vimeungua na biashara za watu wengine zimeungua, viongozi wamefika wamesema tusifanye biashara lakini ni athari kwetu maana wengine tuna mikopo,” alisema.

Makalla aliyekuwepo muda wote katika eneo hilo alisema shughuli ya kuzima moto ilikuwa ngumu kutokana na miundombinu iliyowekwa kuzungukwa na vibanda vya wafanyabiashara.

Zimamoto kukosa maji

Licha ya kuwahi kwenye eneo la tukio hilo magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hayakufua dafu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuishiwa maji.

Jambo lililozua maswali zaidi ni umbali kutoka yalipo Makao Makuu ya Zimamoto (Fire) hadi lililo soko la Kariakoo kuwa m,fupi, takriban kilometa moja, hali ambayo inaaminika isingekuwa shida kwa magari kwenda na kurudi kuchukua maji, lakini iliwachukua saa zaidi ya sita hadi saa 8 usiku kuudhibiti kutokana na kufuata maji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, takriban kilometa 9.7.

Akizungumza katika eneo la tukio hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto, John Masunga alisema kutokana na umbali mrefu wa kufuata maji hayo ilileta ugumu katika kupambana na moto huo.

“Jeshi la Zimamoto tuliwahi kufika katika eneo hili kabla ya saa 3 usiku na kuanza kuzima moto, lakini kwa bahati mbaya eneo hili la Kariakoo mifumo ya maji haifanyi kazi.

“Kutokana na changamoto hii tulikuwa tunaweza kupata maji Airport (uwanja wa ndege) huko ndiko tulikokuwa tunafuata maji, kazi ilikuwa ngumu na tukafanikiwa kuudhibiti saa 8 usiku,” alisema Masunga.

Kutokana na hali hiyo, mwanasiasa na mtaalamu wa kudhibiti na kupambana na majanga, James Mbatia alisema imefika wakati nchi inatakiwa kuendana na kazi ya mabadiliko ya teknolojia kama ambavyo kamati iliyoshiriki kutunga sheria ya kujilinda na kupambana na majanga ya mwaka 2015 ilivyoshauri.

“Hatuwezi kusubiri mpaka matukio yatokee ndipo tuchukue hatua, kuna mengi ya kujiuliza vyombo vya jeshi, bandari vilikuwa wapi kuja kushirikiana na zima moto kudhibiti? Soko la Kariakoo ni nembo yetu. Lakini bado tunajiuliza wafanyabiashara walikuwa na bima? Soko lilikuwa na bima?” alihoji Mbatia.

Soko hilo limeungua wakati kuna uchunguzi unaoendelea dhidi ya waliokuwa viongozi wake ambao walisimamishwa kazi kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ripoti ya CAG ilionya

Moto huo umeibuka kukiwa na tahadhari iliyowahi kutolewa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Machi 2018 kuhusu hatari miongoni mwa majengo ya umma panapotokea hitilafu mbalimbali yakiwemo matukio ya moto.

Imeandikwa na Herieth Makweta, Elizabeth Edward na Fortune Francis.