Mpishi maarufu wa pilau Morogoro afariki dunia
Muktasari:
- Malongoza aliyekuwa mpishi maarufu wa pilau mkoani Morogoro amefariki baada ya kuugua muda mrefu.
Morogoro. Mpishi mashuhuri wa pilau kwenye misiba, sherehe na shughuli mbalimbali za Morogoro na hata mikoa ya jirani Abdalla Malongoza amefariki dunia alfajili ya leo nyumbani kwake baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa ya msiba huo mdogo wa marehemu ambaye pia ni msemaji wa familia Athumani Malongoza amesema Malongoza alianza kuugua mwanzoni mwa mwaka jana na alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo, figo na ini.
Alisema kuwa Malongoza kabla ya kufariki dunia alipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali mkoa wa Morogoro na taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa vijana waliokuwa wasaidizi wa Malongoza Clifon Mtoliela amesema kama kikundi ambacho kilikuwa chini ya marehemu kimepata pigo kubwa kwa kuwa mbali ya kupata kipato kupitia upishi wa pilau lakini pia wameweza kupata ujuzi.
Hata hivyo kwa niaba ya wapishi wenzake wameahidi kumuenzi Malongoza kwa kuendelea kufanya shughuli hiyo ya upishi wa pilau na sehemu ya kipato chao watakuwa wakiipeleka kwa familia ili kusaidia familia aliyokuwa ikimtegemea marehemu.
Miongoni mwa watu waliowahi kupikiwa na Malongoza enzi za uhai katika shughuli mbalimbali Verus Bitaliho amesema kuwa umaarufu wa Malongoza umetokana na ucheshi, uaminifu na ujuzi wake wa kupika pilau tamu.
"Malongoza alikuwa hana makuu alikuwa na uwezo wa kupika kwenye shughuli hata tatu kwa siku na hawezi kuharibu popote, alikuwa mwaminifu hata ukimpa hela za kununua viungo atanunua kwa uaminifu, na pia alikuwa na uwezo wa kugawa chakula hata kama ni kidogo kila mtu atapata," amesema Bitaliho.
Msiba wa Malongoza upo nyumbani kwake Kihonda Idiva manispaa ya Morogoro ambapo kesho atazikwa katika makaburi ya Kola manispaa ya Morogoro.