Mradi wa ikolojia kunufaisha jamii ya waokota matunda Kiteto

Muktasari:

  • Wananchi wa Vijiji vya Amei Loolera, Lembapuli na Losiot, watakaonufaika wa mradi huo na utawezesha jamii hiyo kuendeleza mfumo wa Ikolojia.

Kiteto. Usimamizi Shirikishi wa Mfumo wa Ikolojia utakaotekelezwa na wananchi wa vijiji vinne vya Amei Loolera, Lembapuli na Losiot, chini ya Shirika lisilokuwa la Kiserikali Kinnapa utawezesha jamii hizo haswa ya waokota matunda na wafugaji kuendeleza mfumo wa ikolojia kwa maslahi mapana ya jamii hizo katika vijiji vya ALOLE.

Awali mradi wa SRMP uliwezesha mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi vijiji vya Amei, Loolera, Lembapuli na Lesoit, ambapo sasa mradi wa Usimamizi shirikishi wa mfumo wa Ikolojia utaboresha maeneo ya malisho yaliyotengwa kwa kuweka miundombinu pamoja na uondoaji wa vichaka na upandaji wa nyasi maeneo ya malisho.

Aidha katika taarifa ya mrafi huo iliyotolewa leo kwa wadau wa maendeleo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga Machi 30.2023 imeelezwa mradi huu utawezesha kutambua na kubaini maeneo ya shughuli za kiasili kama vile, maeneo ya matambiko na malisho ya ndama ambayo yalikuwa yanalindwa kwa njia za asili.

Mradi huo utasaidia pia jamii ya kifugaji Masai, kuendeleza mila na tamaduni zao katika maeneo ambayo mradi utayatambua kwa shughuli za kimila.

"Tuna maeneo kama Alalilii, Orupuru, na Amanyataa ambayo kwa jamii ya kifugaji yanaheshimiwa na tunaamini atakaye kiuka taratibu za kimila kuchezea maeneo haya atadhurika" alisema Yohana Oloisiaji (Kiongozi huyo wa mila Kiteto).

“Serikali iyatambue maeneo yetu haya kwani ndio yaliyobeba mila na tamaduni ya kimasai yalitoweka Maasai hatutakuwa tena na mila," amesema Amani Abraham kiongozi wa mila Laigwanani.

Alizungumzia namna watakavyo tekeleza mradi huo, Abraham Akilimali ambaye ni Mratibu wa Shirika la Kinnapa ametaja shughuli zitakazotekelezwa kuwa ni kubainisha maeneo, huku mshauri katika mradi huo akieleza umuhimu wa kutengwa maeneo hayo.

"Mradi wa PEM unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania lengo lake kubwa ni kuwezesha usimamizi shirikishi wa mfumo wa ikolojia kwa jamii za wafugaji na waokota matunda," amesema Kilimali.

Mradi huu utajikita zaidi kusaidia wafugaji na wawindaji waokota matunda kusimamia maeneo ya malisho na kusimamia masuala ya ardhi pia kusaidia kina mama wa jamii hizo kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto.

"Tutashirikiana kubainisha maeneo yaliyotunzwa kwa njia ya asili na kuyapima, kuwezesha vikundi vya vijana usimamizi wa rasilimali kwa maarifa ya asili na teknolojia mpya,” amesema.

Mradi pia utawezesha mabaraza ya kina mama katika shughuli za ujasiriamali rafiki wa mazingira, kuwezesha vikao vya wadau wa masuala ya ardhi na mabadiliko ya tabia nchi kuhusu usimamizi wa rasilimali.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga kufuatia maelezo hayo aliyopata wakati wa kutangazwa mradi huo aliagiza mashirika yote wilayami humo yanayosaidia moja kati ya makundi ya wakulima na wafugaji kuhakikisha kuwa wanayahusisha makundi yote ili kupunguza migogoro.

"Unapotaka kufanya kazi na kundi moja la jamii mfano mkulima hakikisha unamhusha na mfugaji ili aweze kujua mahitaji ya mwezake kinyume chake, hii migogoro ya Kiteto haiwezi kuisha," amesema.

“Elimu hii ni muhimu kipindi hiki cha mabadiliko ya nchi, wilaya yetu ya Kiteto imepokea mifugo mingi kutoka nje maeneo ya jirani. Tuna ngombe laki tano, sasa ukiongeza na zilizoingia tena ni hatari huko wenzetu tunaambiwa wanakimbia ukame, Kiteto kuna nafuu," amesema.