Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msanifu majengo kortini akidaiwa kujipatia Sh788 milioni

Mshtakiwa Alex Temu anayekabiliwa na mashtaka ya kughushi, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya jinai yenye mashtaka matatu.

Muktasari:

  • Temu anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya mwaka 2020, 2023 na mwaka 2025 katika Benki ya KCB Makao Makuu iliyopo katika jengo la Harambee, Wilaya ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Msanifu Majengo, Alex Temu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujipatia Dola za Marekani 299,925 (sawa na Sh788.2 milioni) kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Salome Martin mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.

Akimsomea mashtaka hayo, Wakili Martin alidai kuwa kati ya Julai 17, 2020 na Machi 28, 2023 jijini Dar es Salaam, Temu alighushi azimio la bodi ya kampuni ya Formtech ambalo wakurugenzi wake ni Abdallah Singano na Alex Temu.

Ilidaiwa alighushi azimio hilo kwa lengo la kuonyesha kwamba yeye ni ofisa aliyeidhinishwa kufanya kazi kama mtia saini na ofisa mwenye mamlaka ya kuhamisha na kutoa fedha kutoka kwenye akaunti ya benki ya kampuni hiyo, jambo ambalo alijua siyo la kweli.

Shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa kuwa Oktoba 15, 2025 katika Benki ya KCB Makao Makuu iliyopo katika jengo la Harambee, Wilaya ya Kinondoni, aliwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi akidai ni halisi na imetolewa na kampuni ya Formtech.

Vilevile, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 7, 2021 na Machi 29, 2023 jijini Dar es Salaam, alijipatia Dola 299,925 (sawa na Sh788 milioni) kutoka katika akaunti ya Formtech iliyopo Benki ya KCB, kwa lengo la kuonyesha kuwa yeye ni mtia saini na ofisa mwenye mamlaka ya kutoa na kuhamisha fedha katika akaunti ya kampuni hiyo akijua syoi kweli.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa huyo aliyakana na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi umekamilika.

Hakimu Mbuya aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 7, 2026 kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.

Hata hivyo, mshtakiwa alipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ikiwemo kuwa na wadhamini wawili watakaowasilisha mahakamani fedha taslimu ambazo ni nusu ya mali anayodaiwa kujipatia kwa njia ya udanganyifu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.