Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mshikemshike uchaguzi mdogo wa ubunge, udiwani

Mgombea udiwani wa Kata ya Bagara Mjini Babati Mkoani Manyara, Zebedayo Mathias (Chadema) akiwapungia wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa kata hivyo, baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo kujiuzulu. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vinalalamika kuchezewa rafu 

Dar/mikoani. Mshikemshike wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Buyungu na udiwani katika kata 77 umeendelea kwa vyama na wagombea kukata rufaa, kusubiri uteuzi na kuazimia kwenda mahakamani kupingania haki zao. Uchaguzi umepangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanyika Agosti 12.

Vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vinalalamika kuchezewa rafu katika kata zilizopo Tunduma mkoani Songwe ambako wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa katika kata tano.

Vyama hivyo vimesema vinatarajia kwenda mahakamani kupinga hatua ya msimamizi wa uchaguzi kutowapitisha wagombea wao.

Mkurugenzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia alisema jana asingeweza kuzungumzia malalamiko ya vyama hivyo.

“Uteuzi wa kwanza ulikuwa Julai 14 na wa pili leo (jana) Julai 16 saa 10:00 jioni, baada ya hapo tutaweza kutoa taarifa kamili,” alisema.

Dk Kihamia alisema, “hatuwezi kutoa maelezo nusunusu, sijui kuizungumzia Chadema, na nikifanya hivyo utakuja na kuniuliza tena kuhusu vyama vingine. Kwa hiyo muda ukifika tutatoa taarifa kamili.”

Walia rafu

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema katika kata za Tunduma walikwisha kulalamikia jinsi msimamizi wa uchaguzi alivyoshindwa kupokea majina sahihi ya wagombea wao.

“Kilichotokea Tunduma kila mtu anakijua, tulikwisha kusema mkurugenzi amekataa kupokea majina ya wagombea wetu na kubaki na wale anaowatambua yeye, tumewaagiza mawakili wetu kwenda mahakamani,” alisema Mrema.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu alisema, “chama chetu kitasimama kidete kwa njia za kisheria kuhakikisha wagombea wetu waliopokwa uraia wao wanapata haki yao.”

Chiza aanza na ahadi

Mgombea ubunge wa Buyungu (CCM), Christopher Chiza juzi alianza kampeni akiwaahidi wakazi wa Kata ya Mugunzu kuwa atafanyia kazi kilio chao cha muda mrefu cha kuhamishiwa Wilaya ya Kibondo. Akihutubia mkutano wa hadhara makao makuu ya kata hiyo, Chiza aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuangushwa na Kasuku Bilago (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa 2015, alisema atawasilisha ombi hilo kwa Rais John Magufuli ili lifanyiwe kazi. Uchaguzi unafanyika kutokana na kifo cha Bilago.

Kijiografia, kata ya Mugunzu iko karibu na Wilaya ya Kibondo kulinganisha na Kakonko.

Katibu Chadema ajiuzulu

Katibu wa Chadema wilayani Serengeti, Julius Anthony alitangaza kujiuzulu jana baada ya kutuhumiwa kusababisha mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Ikoma, Kenedy Josephat kutopitishwa. Wakati Anthony akichukua uamuzi huo, uongozi wa wilaya na mkoa wa chama hicho ulitarajia kukutana kujadili sababu za Josephat kushindwa kuwasilisha fomu za uteuzi.

Manyara, Kilimanjaro, Mara

Katika kata tano mkoani Manyara, wagombea wa kata tatu wamepitishwa huku mbili za Tumati na Hayderer wilayani Mbulu wagombea wa Chadema wakiwekewa pingamizi.

Mkoani Kilimanjaro kata tatu za Makanya, Mawenzi na Kelamfua Mokala ndizo zinazofanya uchaguzi na hadi jana jioni hapakuwa na tatizo.

Katibu wa Chadema mkoani Manyara, Gervas Sulle alisema wamepewa barua za kuwekewa pingamizi Daniel Boa wa Hayderer na Zacharia Nihhi wa Tumati.

“Viongozi wa ngazi ya kata walinieleza walijaza ipasavyo fomu zote japokuwa fomu ya mgombea wa Tumati ilikuwa na upungufu lakini ikajazwa upya, tunapinga mapingamizi yao kwa barua,” alisema Sulle.

Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema mgombea wa CCM wa Hayderer, Justin Masuja aliandika barua kumwekea pingamizi Boa wa Chadema na mgombea wa CCM wa Tumati, Paulo Axweso alimwekea pingamizi Nihhi wa Chadema kwa kutojaza ipasavyo fomu. “Baada ya kupitia fomu zilizojazwa na wagombea hao wa Chadema, ofisi yangu imeridhia wamekosa sifa za kugombea udiwani kata za Tumati na Hayderer kwa tiketi ya Chadema,” alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi alisema hadi jana ofisi yake ina mgombea mmoja tu aliyethibitishwa kugombea ambaye ni wa CCM.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola (Dar), Muhingo Mwemezi (Kakonko), Anthony Mayunga (Serengeti), Joseph Lyimo (Babati), Waitara Meng’anyi (Tarime), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi )