Mtazania mmoja anakula kilo 15 za nyama badala ya kilo 50 kwa mwaka

Muktasari:

  •  Serikali ya Tanzania imesema ulaji wa samaki nyama bado uko chini ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mtu mmoja anakula kilo 15 kwa mwaka wakati anatakiwa kula kilo 50.

  

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema ulaji wa samaki, nyama bado uko chini ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mtu mmoja anakula kilo 15 kwa mwaka wakati anatakiwa kula kilo 50.

Hayo yamesemwa leo Alhamis Novemba 25, 2021 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akizungumzia mafanikio ya sekta ya mifugo na uvuvi katika miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Amesema Shirika la chakula duniani (FAO) linashauri mtu mmoja kula samaki kilo 20.3 kwa mwaka lakini ulaji wa kitoweo hicho nchini ni kilo 8.3 tu.

Kwa upande wa maziwa, Ndaki amesema kuwa mtu mmoja anatakiwa anywe lita 200 kwa mwaka lakini hapa nchini mtu mmoja anakunywa lita 54.

“Bado tuko mbali sana tunahitaji kuongeza zaidi,” amesema waziri huyo.

Amesema uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1961 hadi tani 738,166 mwaka 2021.

Amesema kati ya hizo, nyama ya ng’ombe ni tani 508,355.17, mbuzi na kondoo tani 102,137.22, nguruwe tani 41,467.82 na kuku tani 86,205.78.