Mtoto ajinyonga kwa chandarua, matukio yashika kasi

Muktasari:

  • Fahad (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza na mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto wane, amejinyonga kwa kutumia chandarua iliyokuwa kwenye chumba alichokuwa akilala na ndugu zake.

Dar es Salaam. Zimwi la watoto kujikatisha uhai kwa kujinyonga limeendelea kutikisa mwaka 2023 na kuleta taharuki. Miongoni mwa matukio hayo ni la hivi karibuni lililotokea  wilayani Temeke.

Suala hilo linaifanya Desemba 6, 2023 kubaki kwenye kumbukumbu ya familia ya Mikidadi Juma kufuatia kifo cha mtoto wao Fahad Mikidadi aliyepoteza maisha baada ya kujinyonga.

Fahad (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza na mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto wane, alijinyonga kwa kutumia chandarua iliyokuwa kwenye chumba alichokuwa akilala na ndugu zake wengine.

Akizungumza juzi Desemba 6, 2023 na mwandishi wa  Mwananchi msibani nyumbani kwake Mtaa wa Unubini Temeke jijini Dar es Salaam,  baba mzazi wa Fahad, Juma  alieleza kuwa alipata taarifa za tukio hilo akiwa kwenye shughuli zake na hadi sasa haamini kama mtoto wake hayuko naye tena.

“Ni tukio lililonishangaza sijui nini kilimkasirisha kiasi hiki mtoto wangu, asubuhi nimezungumza naye vizuri tukaagana nikaenda kwenye shughuli zangu, jioni napigiwa simu kwamba mtoto amejinyonga,” amesema Juma akitokwa na machozi.

Akisimulia kilichotokea amesema baada ya michezo ya kutwa nzima, Fahad aliambiwa na mama yake aende madrasa, jambo ambalo kwa muda huo hakuwa tayari.

“Inaonekana zile hasira za kuambiwa aende madrasa zikamfanya aingie chumbani na huko ndipo alipokutana na neti akaizunguka kwenye shingo yake, hadi sasa sielewi alijifunza wapi kufanya hivyo kwa sababu si mfuatiliaji wa filamu kusema kwamba ameyaona huko alichokuwa anapenda kuangalia  ni katuni pekee.

“Dada yake ndiye alikuwa  wa kwanza kumuona maana aliingia chumbani na kumkuta akiwa katika mahangaiko, alipiga kelele akiomba msaada ndipo watu wengine walipoingia na kumtoa kwenye kitanzi,” amesema Juma.

Huenda msaada huo ulifika kwa kuchelewa kwani licha ya kumkuta bado akiwa anahangaika kwenye kitanzi hicho cha neti na jitihada za kumuwahisha hospitali umauti ulimkuta wakiwa njiani.

Hata hivyo, Juma amesema hadi sasa hana uhakika kama mtoto huyo alidhamiria kujinyonga au alifanya hivyo akiwa katika michezo yake ya kitoto iliyosababisha kifo chake.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuwa makini na watoto ili kupunguza uwezekano wa kutokea matukio ya aina hiyo, kama lililotokea kwenye familia yake na kusababisha simanzi ya hali ya juu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Gabriel Pupa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanaendelea  na uchunguzi kupata undani wake.

Amesema mazingira ya tukio kama hilo viko vitu vingi ambavyo huwa wanaangalia, ikiwemo mazingira ya tukio muonekano wa kamba ilivyofungwa lakini pia kama marehemu aliacha ujumbe wowote.

"Kimsingi matukio kama haya katika uchunguzi wetu vipo vitu vingi tunavyoangalia, muhimu kabisa ni mazingira ya tukio kama ni kifo cha mashaka, uchunguzi wake utazingatia uhalisia wa tukio," amesema Kamanda Pupa.

Huu umekuwa ni mwendelezo wa wimbi la matukio ya watoto kujinyonga ndani ya mwaka huu yakitokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika kipindi cha miezi 11 gazeti hili limekusanya matukio kadhaa yaliyoripotiwa ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 kujikatisha uhai wao kwa kujinyonga.


Matukio mengine

Februari 10, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Kambarage Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Tatu John (10) alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba chumbani kwake.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mkoani B, Shabani Rashid alipata taarifa za tukio hilo na alipokwenda kwenye nyumba hiyo alikuta marehemu akiwa ameingiza kichwa ndani ya kamba ya neti ambayo imefungwa dirishani.

Hali hiyo ilitokea pia mkoani Mtwara Februari 26, 2023 ambapo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kiromba, Azana Dadi (13), alikutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia mtandio wake kwa sababu alikataliwa kwenda kwenye banda la video usiku.

Taarifa ya polisi ilieleza uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na daktari umebaini chanzo cha kifo ni kukosa hewa, baada ya kubanwa na mtandio shingoni.

Februari 27 mkoani Mbeya mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Lyoto jijini Mbeya, Ibrahim Edson (12) alifariki dunia baada ya kijinyonga kwa kutumia kamba ya katani ndani ya chumba alichokuwa akilala.

Taarifa ya polisi ilieleza kuwa mwanafunzi huyo alifikia hatua ya kujitoa uhai baada ya kufokewa na wazazi wake kwa kuchezea simu ya mama yake hadi kumaliza chaji.

Usiku wa Machi 3, 2023  mtoto wa miaka 10, Dotto ambaye ni mkazi wa kijiji cha Chalinze Mzee wilayani Chalinze, alikutwa amejinyonga baada ya mama yake kumkataza asiende kwenye kigodoro.

Machi 4, 2023 mtoto wa miaka 10, Erick Podi alikutwa amejinyonga eneo la Kisesa jijini Mwanza baada ya kutoweka nyumbani kwa saa kadhaa.

Kwa mujibu wa ndugu wa familia ya marehemu, asubuhi ya siku hiyo mtoto huyo aliulizwa na bibi yake kuhusu madaftari, lakini kabla hajayawasilisha kama alivyoagiza alitoweka na usiku wa siku hiyo alikutwa amejinyonga.

Juni 27,2023 mwanafunzi wa darasa la nne katika Kijiji cha Ikengwa, mkoani Dodoma, Zamada Jafari (13) alifariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia mtandio, chanzo kikidaiwa kukosa nguo ya sikukuu.

Julai 3, 2023,  mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumbira kata ya Luanda wilayani Mbozi mkoani Songwe, Japhari Mwashitete  (16) alikutwa amefariki dunia kwa kujinyonga darasani huku kukiwa na ujumbe wa sababu ya kujinyonga ukieleza kuikataa shule hiyo.

Taarifa ya polisi ilieleza kuwa baada ya kuangalia kwenye mfuko wa suruali ya mwanafunzi huyo na kukuta karatasi yenye maandishi yenye ujumbe wa kukataa kusoma shule ya Lumbira, na badala yake anataka kusoma Shule ya Myovizi iliyopo kilomita chache kutoka shuleni hapo.


Kinachozungumzwa na wadau

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka ameelekeza lawama kwa  wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushindwa kuwalea vema watoto kwa kuwafundisha mema na mabaya, badala yake wanaishia kuwafokea na kuwaadhibu.

“Malezi hayahusishi ukuaji wa kibailojia pekee, yaani kumpa mtoto chakula, lazima uangalie makuzi ya akili na kiroho. Siku hizi wazazi wanafuga hawalei matokeo yake watoto wanayachukua zaidi mambo ya hovyo wanayokutana nayo duniani na kuamini ndiyo sahihi.

“Hayo anayoyachukua yakishajaa kwenye kichwa chake anaanza kujenga chuki kwa wazazi wake kwamba akiambiwa au kufokewa anaona kaonewa anaona bora ajiue,” amesema.

Mwanasaikilojia Jonas Kinanda amesema baadhi ya wazazi wanachangia kwenye matukio ya watoto kujidhuru kutokana na maneno mabaya wanayowatolea ikiwemo ya kuwafananisha na wanyama.

“Unakuta mzazi anamuita mtoto wake majina ya wanyama kwa uelewa wa watoto wa sasa wanaona wametukanwa na kuamua kuchukua maamuzi maagumu ya kuondoka nyumbani au kujiua, na hasemi sababu ya kuchukua maamuzi hayo,” amesema Kinanda.

Amesema kuna haja ya wazazi kubadilika na kuacha tabia ya kuwaita watoto majina tofauti na waliyowapa ili kuepusha masononeko na kujiona hawana thamani ya kuishi. Pia amesema wazazi wamjengee mtoto tabia ya kuelezea hisia zake pale anapokutana na hali ambayo si ya kawaida iwe vitu vya shule au nyumbani.

Hilo limethibitishwa na Salma John (si jina halisi) anayeeleza kuwa maneno aliyokuwa akipewa na mama yake akiwa mtoto kuna wakati yalimfanya atamani kujikatisha uhahi, kwa kile alichoamini kuwa hapendwi.

“Nakumbuka nikiwa darasa la saba siku moja mama alinitolea maneno makali, nikahisi kabisa sipendwi na sitakiwi kuwepo duniani, hivyo nikaingia chumbani nikaandika barua kwamba najiua kwa sababu mama hanipendi kama anavyowapenda ndugu zangu wengine. Baada ya kuandika ujumbe nikachukua kanga na kutengeneza kitanzi nikaanza kujikaba shingoni, maumivu niliyopitia yalinifanya nisitishe kitendo hicho na kuchana ule ujumbe, hadi leo hakuna anayefahamu kama niliwahi kufanya jaribio hilo,” amesema.

Restituta Jeremia mkazi wa Temeke  ameshauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuwepo kwa walimu au wataalamu wa saikolojia kuanzia elimu ya msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu, ili kudhibiti matukio yaliyoshamiri kwa watu kuchukua hatua za kujikatisha uhai kutokana na kuwepo kwa msongo wa mawazo.

“Hawa watoto wanaojinyonga ni wadogo inapaswa kuitafakarisha jamii na huenda kuna mambo mengi nyuma ya pazia, sisi tunasikia tu mtoto amejinyonga. Kuna haja ya wazazi na walezi kuwa makini na kuzungumza kwa ukaribu na watoto katika familia, pindi inapojitokeza changamoto ili kuwaepusha kuchukua maamuzi magumu ya kujitoa uhai,” amesema Restituta.