Mtoto mbaroni akituhumiwa kumuua baba yake Dar, afukia mwili chumbani
Muktasari:
- Juma Ramadan (21), maarufu Juli, atiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Ramadan Jafar (47), maarufu Muna, kisha kwenda kuufukia mwili wake kwenye moja ya vyumba alivyokuwa akikitumia baba yake.
Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imemtia mbaroni Juma Ramadan (21), maarufu Juli, mkazi wa Ubungo, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Ramadan Jafar (47), maarufu Muna, ambaye awali aliripotiwa kupotea.
Kwa mujibu wa polisi, baada ya kudaiwa kufanya mauaji hayo, polisi ilieleza kuwa mtuhumiwa alichimba shimo ndani ya moja ya vyumba vya nyumba hiyo na kuufukia mwili wa baba yake, ambaye kabla ya kifo chake alikuwa akitumia chumba hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Jumanne, Juni 23, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema Juni 16, 2026, Kituo cha Polisi Kimara Gogoni kilipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Ramadan Jafar kuhusu kupotea kwake.
Muliro amesema baada ya taarifa hiyo kupokewa, uchunguzi ulianzishwa kwa kushirikisha vitengo mbalimbali vya Jeshi la Polisi pamoja na wananchi.
Amesema uchunguzi huo ulibaini mtu aliyeripotiwa kupotea alikuwa ameuawa na mwili wake kufukiwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumba yake iliyopo Mbezi Luguruni Kwembe, Wilaya ya Ubungo.
“Uchunguzi wa awali ulionyesha mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa mtoto wa marehemu, ambaye naye alikuwa ametoweka baada ya tukio hilo,” amesema Muliro.
Amesema juhudi za upelelezi ziliwezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa katika eneo la Msufini, Msoga, mkoani Pwani. Baada ya kuhojiwa, polisi ilieleza kuwa mtuhumiwa alidaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo na kueleza jinsi alivyotekeleza tukio hilo kabla ya kuufukia mwili wa baba yake.
Kamanda Muliro amesema chanzo cha tukio hilo bado kinaendelea kuchunguzwa na vyombo vya usalama ili kubaini sababu zilizomfanya mtuhumiwa kutenda kitendo hicho cha kikatili.
Amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linalaani tukio hilo pamoja na vitendo vingine vya uhalifu, na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya uhalifu.
“Tunawahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama, kwani wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema Muliro.