Mtwara waomba kujengewa hosteli

Thursday June 23 2022
mtwaraapic
By Florence Sanawa

Mtwara. Baada ya wanafunzi wanne kunusurika kifo katika ajali ya bodaboda mkoani Mtwara, mkuu wa shule ya sekondari Mangamba, Said Mpate ameomba wadau wa serikali kuwajengea hosteli.

Ametoa kauli hiyo mbele ya rais wa shirika la Wentworth, Barbara Bean katika uzinduzi wa maktaba ya shule hiyo iliyofanyiwa ukarabati na shirika la realizing education for Development (Read) Tanzania kwa ufadhili wa Wentworth Africa Foundation ambapo waligawa na taulo za kike kwa wanafunzi zaidi ya 300.

Amesema wanafunzi hao wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita 18 huku asilimia 80 wakiwa wanaishi Mtwara mjini.

Amebainisha kuwa wengi wao hupanda bodaboda na wengine hulazimika kutembea kwa miguu kutokana na shida ya usafiri wa kufika shuleni hapo.

Naye mkurugenzi wa Read Tanzania, Rebecca Liundi amesema wamefanikisha kukarabati jengo hilo kwa ufadhili wa Went Worth Afrika Foundation na kuweka vitabu 954 na thamani mbalimbali zikiwemo meza na  viti, kompyuta  pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali kwa watoto na walimu ambapo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 33.

“Jamii ya Mangamba inajua kuwa tumepata maktaba tulichukue kama fursa ili kuhakikisha kuwa makataba na vitabu vinatunzwa  na vinatumika katika hali nzuri  kwa mafanikio ya watoto wenu na vizazi vijavyo pia natamani kuona kiwango  cha usomaji kwa wanafunzi na kiwango cha ufadili kimeongezeka," amesema.

Advertisement

Geofrey Kituye, ofisa elimu taaluma wa Mkoa amesema kuwa kitendo cha kuichagua shule hii ambayo ni miongoni mwa shule nyingi zilizopo katika mkoa huu ni jambo la kusimamia na kuitunza.

Advertisement