Muhimbili yamwekea mgonjwa taya jipya
Muktasari:
- Timu ya wataalamu wazawa wa Muhimbili imefanya upasuaji wa kwanza wa kutengeneza taya. Huduma hiyo imehusisha upasuaji wa aina tatu kwa wakati mmoja.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanya upasuaji wa kuvuna kipande cha ubavu kilichotumika kama kiungio cha fuvu kwa ajili ya kumtengenezea mgonjwa taya jipya.
Huduma hiyo ya kibingwa imefanyika kwa mgonjwa ambaye taya lake limeathiriwa na uvimbe, hivyo kuhitaji kuwekewa taya jipya.
Upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini, ni mwendelezo wa utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi unaotokana na kujenga uwezo wa watalaamu wazawa.
Akielezea upasuaji huo, daktari bingwa wa upasuaji wa uso na taya, Arnold Augustino amesema umehusisha kuondoa taya lote la upande wa kulia na kutengeneza taya jipya.
Amesema mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji aina tatu tofauti kwa wakati mmoja wa kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe ambapo umechukua saa saba umeshirikisha timu watalaamu wa Muhimbili.
“Mgonjwa huyu amefanyiwa upasuaji wa kuondoa taya lote la kulia iliyoathiriwa na uvimbe na hivyo kumtengenezea taya jipya kwa kuchukua mfupa kutoka kwenye ubavu ambapo mfupa huo umepandikizwa kwenye kiungio cha taya,” amesema.
Ameongeza kuwa mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye nyonga pande zote mbili, ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalumu kutengeneza sehemu ya taya iliyoharibika na ugonjwa.
Dk Augustino amebainisha baada ya upasuaji huo mgonjwa anategemea kuendelea kula na kutafuna kama kawaida, kwani atawekewa meno bandia kwenye mfupa wa taya aliotengenezewa.
Timu ya wataalamu 10 ilihusika kwenye upasuaji huo ikihusisha madaktari bingwa wa taya na uso watano, wataalamu usingizi na ganzi wawili, manesi wa upasuaji watatu na madaktari wanaosomea ubingwa wa kupasua mataya na uso.