Mukherjee: 'Mwalimu ndiye msingi wa fani zingine'

Dar es Salaam. Wazazi, walezi pamoja na walimu nchini wametakiwa kuwahamasisha watoto wao kusomea fani ya ualimu huku akichagiza kuwa hiyo ndio mama wa taaluma zote duniani.

Wito huo umetolewa leo Juni 8, 2024 na Mkuu wa Shule ya Sekondari Aga Khan Mzizima Dk Arun Mukherjee katika hafla iliyokutanisha wahitimu mbalimbali waliosoma shule hiyo tangu ilipoanzishwa.

Mukherjee amesema ualimu ni mojawapo ya fani adhimu na muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote lile duniani na hakuna fani inayoweza kuwepo bila ya mwalimu.

Hata hivyo amesema miaka ya hivi karibuni  vijana wengi wamekuwa wakipendelea kusoma fani nyingine kama vile uhasibu, udaktari na nyinginezo.

Amesema pamoja na kuwa fani hizo zina umuhimu sana katika ustawi wa jamii lakini ili ziendelee kuwepo zinahitaji uwepo wa mwalimu.

"Kila mmoja wetu anatambua umuhimu na michango ya walimu katika maisha yake ya kila siku, hivyo nawasihii kuiangalia pia taaluma hii ambayo ndio msingi wa taaluma zote duniani"amesema.

Kwa upande wake Mwanamuziki wa kizazi kipya ambaye pia ni moja kati ya wahitimu waliosoma shule hiyo,  StaraThomas alitoa wito kwa shule mbalimbali kugeukia fursa zilizopo katika sanaa kwani ni moja kati ya sekta ambayo inazalisha ajira kwa vijana wengi.

Anasema kama sanaa nayo itapewa nafasi ya kufundishwa ipasavyo mashuleni itawasaidia watoto wenye vipaji kuendelea kupata elimu huku wakikuza vipaji vyao hivyo kuwasaidia hata wanapohitimu kujiajiri kupitia vipajo vyao.

"Sanaa nayo ina nafasi katika kumjenga vizuri mtoto kama itafundishwa kwa ukamilifu mashuleni"amesema.

Akizungumzia hafla hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda ambaye alikuwa mgeni rasmi na mhitimu kutoka katika shule hiyo amesema ni muhimu kwa watu waliosoma pamoja kuweka utaratibu wa kukutana kwani inasaidia kujenga ushirikiano pamoja na undugu baina yao.

Nae Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Aga Khan Education Service Tanzania, Shabir Abji amesema shule hiyo inatarajia kufanya mabadiliko makubwa ikiwemo ujenzi wa madarasa pamoja na ukarabati wa madarasa yaliyopo kuyafanya ya kisasa zaidi.

Pia uboreshaji wa maabara, maktaba pamoja na vyumba vya komputa kufanya kuwq bora zaidi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo sasa ikilenga kuboresha zaidi elimu wanayoitoa