Mume adaiwa kuua mke kisa ng’ombe
Muktasari:
- Mkazi wa Kijiji cha Muwara, wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro, Magdalena Makishe (61) amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na mumewe, Zakayo Kimaro anayetuhumiwa kuuza ng’ombe wa kulimia (maksai).
Siha. Mkazi wa Kijiji cha Muwara, wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro, Magdalena Makishe (61) amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na mumewe, Zakayo Kimaro anayetuhumiwa kuuza ng’ombe wa kulimia (maksai).
Kifo hicho kilitokea Aprili 17 mwaka huu, baada ya Magdalena kupigwa Machi 31, kwa madai kuwa aliuliza alipo ng’ombe wake ambaye hakumkuta aliporejea kwenye shughuli zake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale alisema, “ni kweli mama huyu alishambuliwa na mume wake kwa sababu za kifamilia, amefariki dunia na huyu baba aliyemshambulia yuko mikononi mwa polisi akisubiri kujibu tuhuma za mauaji kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.”
Akisimulia tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Godchance Moshi alisema mwanamke huyo alikuwa na ng’ombe wawili wa kulimia, mmoja alikuwa ni wake na mwingine alikuwa ni wa mtu mwingine.
Alisema baadaye alimpumzisha ng’ombe wake kuendelea na shughuli za kulima.
“Ng’ombe wake alivyokuwa akitumika, akaona ndivyo sivyo, akamsimamisha ili asilime tena, apumzike kwanza amlishe ili aweze kununua madume mawili,” alisema Godchance.
“Huyu ng’ombe akiwa amepumzishwa hapo nyumbani, mume wake akawa analazimisha kumuuza lakini mama akakataa, mume wake na kijana wake wakalazimisha kumuuza ng’ombe kwa nguvu wakati huyu mama akiwa sokoni kwenye shughuli zake.
“Aliporudi nyumbani alipouliza ng’ombe wake yuko wapi, akapigwa na fimbo nene mgongoni na sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema Godchance.
“Alipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu lakini baadaye aliruhusiwa, japo aliendelea kuumwa ikabidi apelekwe kwa kaka yake lakini alifariki dunia.”
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwa taratibu za mazishi.