Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma kutua rasmi bungeni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 16, 2026 wakati wa Kikao cha Kumi cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13 jijini Dodoma.
Muktasari:
- Fedha hizo ziliombwa leo Alhamisi Aprili 16,2026 na Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti bungeni jijini Dodoma.
Dar es Salaam. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), imeliomba Bunge kuidhinishia Sh144.85 bilioni ili kutekeleza mambo matano likiwemo la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Dira 2050.
Mengine ni kuhamasisha, kuwezesha na kutoa huduma kwa wawekezaji wa sekta binafsi, kuimarisha uwekezaji wa umma, kuimarisha mazingira biashara na uwekezaji na kuratibu programu za kuondoa umaskini.
Fedha hizo ziliombwa leo Alhamisi Aprili 16,2026 na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti bungeni jijini Dodoma.
Profesa Kitila amesema katika kutekeleza Dira 2050 na nyenzo zake, Tume ya Taifa ya Mipango itaandaa Mwongozo wa Taifa wa Tafiti na ubunifu ili kuweka utaratibu utakaowawezesha watafiti na wabunifu kufanya shughuli zao na kuchangia kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wa mipango.
“Kutayarisha Mfumo wa Kidijitali wa Tafiti ili kuhifadhi tafiti na kuchakata matokeo ya tafiti na kuibua mikakati ya kuzitumia kuleta mageuzi kiutendaji na kiutekelezaji na kufikia malengo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano,” amesema Profesa Kitila.
Kuhusu uhamasishaji, kuwezesha na kutoa huduma kwa wawekezaji wa sekta binafsi, Profesa Kitila amesema Serikali itafanya tathmini ya utekelezaji wa vivutio vilivyopo ili kubaini ufanisi wake na maeneo yanayohitaji maboresho.
“Msisitizo utawekwa katika kuhakikisha kuwa vivutio hivyo vinachochea uwekezaji mkubwa wa kimkakati unaoweza kuleta mageuzi ya viwanda, kukuza viwanda vidogo na vya kati, na kuongeza ajira kwa vijana,” amesema.
Aidha, Profesa Kitila amesema Ofisi ya Tume ya Mipango kwa kushirikiana na wadau itaandaa mkakati wa kuvutia uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya uunganishaji na utengenezaji wa magari.
“Shabaha yetu ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe kinara wa uzalishaji na uunganishaji magari barani Afrika,” amesisitiza.
Pia, amesema Serikali itatenga maeneo maalumu ya uwekezaji kwa ajili ya vijana kupitia programu ya ‘maeneo maalumu ya uwekezaji’ yaliyopo mikoa ya Dodoma, Pwani, Mara, Singida na Ruvuma ili kuwawezesha kuwekeza iwe binafsi au kwa vikundi.
Muswada wa Sheria ya
Uwekezaji wa Umma mbioni
Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji wa umma, Serikali imepanga kukamilisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma kwa mwaka wa fedha 2026/27, ili kuboresha utendaji wa taasisi na mashirika ya umma yajiendeshe kwa tija, kuongeza mapato ya Serikali na kuchangia utekelezaji wa Dira 2050.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila, muswada huo unalenga kuweka mfumo mpya wa kisheria wa usimamizi wa uwekezaji wa umma, utakaosaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa Taifa.
Amefafanua kuwa muswada huo utapendekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma itakayoratibu na kusimamia uwekezaji wa Serikali kupitia taasisi zake kwa mtazamo wa kitaifa.
“Utapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma utakaosaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji kupitia mashirika ya umma, bila kuhatarisha vyanzo vya msingi vya mapato vinavyoingia katika mfuko mkuu wa Serikali,” amesema.
Pia, Serikali inalenga kuongeza uhuru wa kiutendaji kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara, ili kuyawezesha kujiendesha kwa tija zaidi, kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali na kuimarisha ushindani katika sekta zake.
Profesa Kitila amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 Serikali itaendelea na mchakato wa tathmini ya kina ya utendaji wa mashirika na taasisi za umma, akisema itachukua hatua stahiki ikiwemo kuunganisha taasisi na mashirika yenye majukumu yanayofanana.
“Tutayafuta yale ambayo malengo yake yamepitwa na wakati au majukumu yake yanaweza kutekelezwa na taasisi nyingine, pamoja na kuboresha yale yenye changamoto za kiutendaji,” amesema.
Maoni ya kamati
Katika hatua nyingine, Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria, imetoa mapendekezo mbalimbali kwa wizara hiyo ili kuboresha utendaji na ufanisi wa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji).
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Damas Ndumbaro imeitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuongeza kasi ya usimamizi wa mashirika ya umma ili kuhakikisha yanachangia ipasavyo mapato ili kufikia lengo lililowekwa katika bajeti ya mwaka 2026/27.
Dk Ndumbaro amesema kamati hiyo imeishauri Serikali kuanza uratibu wa kuwapata wakurugenzi wakuu na wajumbe wa bodi kwa njia ya ushindani mapema iwezekanavyo, ikiwemo kuweka wazi orodha ya mashirika ya umma ambayo yatapaswa kutumia mchako wa huo.