Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muumini aishi na maiti ya mchungaji miezi miwili akisubiri afufuke

Muktasari:

  • Inasemekana mwili wa mchungaji tangu Oktoba ulikuwa ukioshwa, kubadilishwa nguo na kufunikwa kwa chandarua.

Iringa. Muumini wa Kanisa la El-Huruma (E.H.C), Agnes Mwakijale, anashikiliwa na polisi mkoani hapa, akidaiwa kuishi na maiti ya mchungaji wake, John Chida kwa miezi miwili akiamini angefufuka.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata Mchungaji Chida alifariki dunia Oktoba lakini mwili wake uligunduliwa Desemba 3, 2024 ndani ya nyumba yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allen Bukumbi hajapatikana kuzungumzia tukio hilo.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela amethibitisha kupokea mwili wa Chida uliokuwa umeharibika.

“Mwili ulikuwa umeharibika mno. Mwanamke aliyekuwa akiuhudumia anapimwa kubaini kama ana changamoto ya afya ya akili,” amesema.

Amesema mwili umehifadhiwa hospitalini hapo kwa taratibu zaidi, huku uchunguzi ukiendelea.

Awali, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isakalilo ‘C’, Kata ya Kalenga, Amos Msole akizungumzia tukio hilo amesema Desemba 4,2024 alipokuwa akitoka shambani, alipita kwenye nyumba ya mchungaji huyo.

“Nilikutana na mwanamke nikamuuliza mchungaji yuko wapi. Alisisitiza kuwa alikuwa akipumzika. Nilipoingia ndani, nilikuta mwili wake umeharibika, huku kukiwa na harufu kali.”

Amesema aliujulisha uongozi wa kata na Polisi, hivyo Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) alituma askari waliofika kuchukua mwili huo.

“Nilipomuuliza mwanamke huyo kwa nini hakutoa taarifa, alidai mchungaji hakuwa amekufa bali Mungu alikuwa amemchukua kwa muda na angeweza kumrudisha,” amedai.

Msole amedai mchungaji huyo alikuwa mtu wa kujitenga na madirisha ya nyumba yake yalikuwa yakifungwa hivyo kuwa vigumu kugundua iwapo amekufa.

Amewasihi wananchi kuripoti magonjwa au hali zisizo za kawaida kwa viongozi wa eneo husika ili kuepusha matukio kama hayo.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema walikuwa wakimhudumia mchungaji tangu Oktoba kwa kumuosha mwili kila siku, kumbadilisha nguo na kumfunika kwa chandarua kama alivyoagiza kabla ya kifo chake.

Mchungaji Chida inaelezwa kuwa alihamia kijijini hapo mwaka 2022 akijitambulisha kuwa muhubiri kutoka mkoani Tanga.

Msole amedai alieleza alikuwa na mpango wa kufungua tawi la Kanisa la El-Huruma.

Amedai afya ya mchungaji huyo ilianza kudhoofu Agosti 2024 baada ya kurejea kutoka Mwanza.

Amesema Julai mchungaji huyo alisafiri kwenda Mwanza na aliporejea Agosti afya yake haikuwa nzuri.

Amedai alipokutana naye wakati wa ufunguzi wa barabara ya Lipuli iliyo jirani na kanisa lake alibaini kwamba ni mgonjwa, hivyo alimshauri aende hospitali.

Amedai mchungaji huyo alimweleza afya yake imeimarika na Mungu atampa uponaji.

“Siku zilivyozidi kwenda afya yake ilikuwa inadhoofu ndipo nikamwambia mtumishi wewe unaumwa naomba nikupeleke hospitali, alikataa,” amedai.

Mwanasaikolojia Leonard Mgina, mkazi wa mjini Iringa amesema alichofanya muumini huyo kuishi na maiti kwa muda huo kinaashiria ana changamoto ya afya ya akili.

“Aliishi na mwili huo kwa miezi miwili, jambo linaloashiria matatizo ya kisaikolojia,” amesema.