Mvua ilivyoleta uharibifu, maafa
Muktasari:
- Kwa mujibu wa TMA, kuna uwezekano wa mvua kuongezeka maradufu na inatarajiwa kuendelea kunyesha hadi mwishoni mwa mwezi huu.
Dar/Mikoani. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa tahadhari kwamba mvua haitarajiwi kupungua katika siku za karibuni, madhara yameripotiwa katika maeneo kadhaa nchini vikiwamo vifo vya watu watatu na uharibifu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa TMA, kuna uwezekano wa mvua kuongezeka maradufu na inatarajiwa kuendelea kunyesha hadi mwishoni mwa mwezi huu.
Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi juzi alisema mvua zitaendelea kunyesha katika viwango tofauti kutokana na mambo mengi ikiwamo mabadiliko katika bahari.
Madhara Tabora
Wananchi 3,800 wa Kata ya Usinge wilayani Kaliua mkoani Tabora hawana makazi baada ya nyumba zao kuathiriwa na mvua.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kaliua, Dk John Pima katika taarifa aliyoitoa kwa baraza la madiwani mwishoni mwa wiki alisema nyumba 691 zimeathiriwa.
Alisema nyumba 414 kati ya hizo zimeanguka, huku nyingine zikibomoka na kupata nyufa kubwa hivyo kuwalazimu waathirika kupewa hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Dk Pima alisema, “kwa takriban siku 10 sasa, waathirika hao wanaishi kwa ndugu, lakini katika kuwanusuru na maradhi ya mlipuko wamepeleka dawa na wataalamu wa afya.”
Katika Kata ya Usinge, visima na vyoo vimeathiriwa na mvua hivyo kusababisha maji kuchafuka.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Kaliua, Haruna Kasele alisema wananchi hao wanahitaji msaada.
Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alitaka taarifa ziwasilishwe haraka ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa ili kuona jinsi ya kuwasaidia waathirika hao.
Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema uharibifu uliosababishwa na mvua katika mkoa wake ni mkubwa na wanafanya utaratibu wa kuwatafutia walimu maeneo ya kuishi karibu na shule.
Kaya 66 zinakabiliwa na uhaba wa chakula mkoani Kilimanjaro baada ya nyumba zao kuanguka na kusombwa na maji ya mvua.
Mghwira alisema kaya hizo zinahitaji msaada wa chakula.
Alisema mvua imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara, shule na mashamba.
Mghwira aliyataja maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mvua kuwa ni kata za Makuyuni, Mabogini, Okaoni, Mikocheni na Arusha Chini zilizopo Moshi Vijijini na kata ya Kileo iliyopo wilayani Mwanga.
“Katika kata hizo nyumba zilizobomoka ni 180 na vyoo 86. Kaya 66 zimekosa makazi na watu watatu wamekufa,” alisema Mghwira.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi walisema kuharibika kwa miundombinu ya barabara kumesababisha bei ya chakula na nauli kupanda.
Rukia Musa, mkazi wa Kijiji cha Mikocheni, Kata ya Arusha Chini alisema, “Baadhi ya wanafunzi na walimu wanaotoka maeneo haya kwenda shule za mbali au wanaokuja shule za hapa hawaendi shule, kwa zaidi ya wiki mbili sasa, na hii ni kutokana na barabara kuharibika.”
Alisema mvua imesababisha hali ya maisha kuwa ngumu, akisema kilo ya unga wa sembe inauzwa Sh2,500 kwa kile ambacho wafanyabiashara wanasema ni gharama za usafirishaji.
Alisema gharama za usafiri zimepanda kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000 kwa mabasi na bajaji, huku wafanyabiashara wanaotumia pikipiki wakilipa Sh10,000.
Ally Juma, mkazi wa kitongoji cha Kirungu aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa msaada kwa wakazi wa eneo hilo, ikiwamo kuboresha miundombinu ya barabara.
Wahofiwa kufa Pwani
Mkoani Pwani, watu watano akiwemo raia wa Marekani aliyetajwa kwa jina moja la Kenneth wanahofiwa kufa maji baada ya mtumbwi kupigwa na dhoruba eneo la Nyamisati wilayani Rufiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rufiji, Onesmo Lyanga akizungumza na Mwananchi alisema tukio hilo lilitokea Mei 3 saa mbili asubuhi, watu hao walipotokea Kibiti kuelekea Mafia.
Alisema watu watano pamoja na mtumbwi hawajulikani walipo. Alisema nahodha aliyetajwa kwa jina moja la Mambo alinusurika na alifika kisiwani Kome.
Kamanda Lyanga alisema nahodha huyo aliokolewa na wavuvi na alipelekwa kwa matibabu katika hospitali ya Mafia.
Alisema wanaendelea kuwatafuta watu hao na taarifa zitaendelea kutolewa kadri itakavyowezekana.
Imeandikwa na Robert Kakwesi (Tabora), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi) na Sanjito Msafiri (Pwani).