Mvua yaathiri shughuli mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma

Muktasari:

  • Miundombinu ya bandari ndogo ya Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji yaharibiwa na mvua.

Kigoma. Mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali mkoani hapa zimesababisha maji kujaa kwenye mwalo na kuharibu miundombinu ya bandari ndogo ya Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Hali hiyo imesababisha kukwama kwa shughuli za kibiashara ndani ya Mkoa wa Kigoma na nchi jirani.

Wakizungumza leo Machi 19, 2024 wafanyabiashara katika mwalo huo na eneo la bandari wamesema Serikali iboreshe eneo hilo ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato.

Mfanyabiashara mwaloni hapo, Hassan Juma amesema changamoto ya kujaa maji eneo hilo inakwamisha biashara, hivyo Serikali ione umuhimu wa kuchukua hatua haraka.

Msafirishaji wa samaki na dagaa, Zetrida Ezekiel ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya soko kwa wakati ili maji yakiongezeka yasiweze kuwaathiri.

Msafirishaji wa mizigo na abiria kwenda maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, Issa Mustapha amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi mvua bado zinaendelea kunyesha, hivyo ni muhimu Serikali ikaongeza nguvu katika kuboresha bandari kutokana na maji kujaa, hivyo shughuli za usafirishaji kukwama.

“Gati limejaa maji, inakulazimu kutembea na mzigo mita kadhaa ukiwa umeubeba ili kuingiza ndani ya boti, hatua hii inaweza kusababisha hasara kwa wenye mizigo endapo utaangukia kwenye maji,” amesema Mustapha.

Kaimu Ofisa Biashara wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kanyama Kalombo amesema wanaendelea na mchakato wa kuwaandalia wafanyabiashara hao maeneo ya kufanyia shughuli zao kwa muda.

Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Kigoma, Silvester Mabula amesema maji hayo yamejaa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema wamejipanga kufanya tathmini na kuangalia njia mbadala ili wateja wao na wananchi waendelee kupata huduma kama awali.

“Kutokana na hali hiyo, TPA haijakaa kimya inaangalia njia mbadala kuhakikisha huduma za wateja zinaendelea kufanyika kama kawaida,” amesema na kuongeza:

“Tunafanya tathmini ya gharama zinazohitajika kuangalia upande mwingine wa bandari kwa ajili ya kutengeneza njia nyingine ambayo wataitumia wateja wetu,kwani eneo hili ni muhimu sana kwetu,” amesema Mabula.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Pia amewataka wafanyabiashara wa samaki na dagaa wa eneo hilo kuhama kwa muda kutokana na maji kuongezeka katika eneo lao la biashara.

“Katika wilaya yetu tuna masoko mengi, niwaombe muhamie huko kwa muda ili mwendelee kufanya biashara na kupaacha wazi hapa ili tupaboreshe, maji yakiongezeka wakati mwingine yasiweze kufika eneo hilo,” amesema Kalli.

Amesema hakuna sababu ya wafanyabiashara kupanga biashara barabarani kwani masoko yapo ya kutosha.