Mvua yakwamisha waumini kuswali Sikukuu ya Eid Tanga

New Content Item (2)

Baadhi ya waumini wa dini ya Kiisalam walioswali swala ya Eid El Fitr msikiti mkuu wa kata Vibaoni, wakitafuta viatu vyao ambavyo vilivyosombwa na maji baada mvua kunyesha leo Jumamosi Aprili 22, 2023 wilayani Handeni mkoani Tanga. Picha na Rajabu Athumani.

Muktasari:

  • Ibada ya Swala Eid El Fitr inafanyika kwa waumini wa dini ya Kiisalamu baada ya kukamilisha funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni moja ya nguzo tano ya dini hiyo.

Handeni. Waumini wa dini ya Kiislamu katika baadhi ya maeneo mkoani Tanga imewabidi kubanana ndani ya misikiti na wengine kuswali pembeni ya misikiti kutokana na mvua kunyesha na kushindwa kuswali katika viwanja vya misikiti.

Hali hiyo imetokea leo Jumamosi Aprili 22, 2023 katika maeneo ya Tanga mjini, Handeni, Korogwe na sehemu nyingine za mkoa huo, baada ya mvua kunyesha na kusababisha viwanja vingi vya misikiti kulowana maji.

Mmoja wa waumini hao, Nurudin Hamza amesema ibada imekuwa na baraka ya mvua, ila ni changamoto kwa wengine kwani wameshindwa kutoka katika nyumba zao kwenda msikitini.

Amesema kwa kuwa ni muda mrefu watu wamekuwa kwenye kipindi cha ukame mvua hiyo wanaona ni kama baraka, kwa sababu hata wale waliopanda mazao inaleta matumaini kwao.

"Watu wametoka kwenye ibada msikitini hawaoni viatu vyao, vimesombwa na maji tumekwenda kuviokota nyumba za jirani na msikiti na wengine wamekwenda pekupeku nyumbani kutokana na viatu kwenda na maji," amesema Omar Hojoro mkazi wa Vibaoni.

Hata hivyo ibada iliendelea kwa watu waliofanikiwa kuingia ndani msikitini, huku wachache wakiswali katika Baraza ya Msikiti wakiwa wameolowana.

Imamu Msikiti Mkuu wa Kata ya Vibaoni, Kombo Nkucha katika ibada hiyo ya swala ya Eid El Fitr amewataka waumini hao, kuhakikisha utaratibu wa kutoa msaada kwa wasiojiweza unaendelea licha ya funga kukamilika.

Amesema kuwa baadhi ya waumini mwezi wa Ramadhan ukimalizika wanaacha kufanya ibada lakini pia, hata yale matendo mema yanakuwa ndio mwisho wake, jambo ambalo siyo sahihi.

Msoma hotuba ya Msikiti Mkuu wa Vibaoni, Omar Mafuli katika nasaha za Eid El Fitr amewataka waumini hao kuacha kuitumia sikukuu hiyo kufanya maasi, kwani kufanya hivyo ni kuharibu ibada waliofunga mwezi mzima.

Amekemea tabia ya kufanya yale yote ambayo dini inakataza na waliaacha kipindi cha mwezi wa Ramadhan hasa suala la uzinifu na baadaye wengine kuja hata kupata mimba na kuzitoa.

"Leo kuna watu wameshawekeana ahadi ya kukutana na kwenda kufanya zinaa, mbaya zaidi hao watu ikipatikana mimba wanakuja kuitoa na kuua kiumbe asiye nanhatia, kitu ambacho ni dhambi mara mbili, tuepuka zinaa na utoaji mimba mungu yupo siku zote," amesema hatwibu Omar.

Sikukuu ya Eid El Fitr inafanyika ambapo kila muumini anatakiwa kutoa Fitr ambayo ni chakula au fedha kwa watu wasiojiweza ili kukamilisha swaumu yake.