Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu Fatma, aeleza mbinu tatu za kuishi ndoa ya ukewenza

Kama ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii, hasa Instagram, inawezekana umeshakutana na video fupi inayozungumzia masuala ya kuishi vyema katika ukewenza kutoka kwa Mwalimu Fatma Mdidi.

Video hizo ‘zilitrend’ sana miezi kadhaa iliyopita kutokana na watu wengi kushuhudia namna ndoa za ukewenza zinavyozua tafrani.

Baadhi ya wanawake waliopo kwenye ukewenza wamekuwa wakirushiana vijembe, kushikana uchawi na hata kufikia hatua ya ndoa kuvunjika ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, hili halijatokea kwa Fatma, ambaye tangu aolewe ndoa hizo za mitala, yapata mwaka wa 22 sasa anaishi vizuri tu na wakewenza.

Fatma, ambaye ni mtoa mihadhara ya dini ya Kiislamu maarufu, amefanya mahojiano ya kina na Mwananchi na kueleza siri ya kudumu kwake, huku akitoa somo la namna ya kuishi kwa wanaume wanaotaka ndoa za mitala na wanawake wanaoingia kwenye ndoa hizo.
 

Maisha yake kifamilia

Fatma ambaye ni mwalimu wa masomo ya sayansi na dini, anasema ili mwanamke adumu kwenye ukewenza ni lazima aishi maisha yake mwenyewe (aache vita), mwanamume awe mwadilifu wa kutenda haki kwa wake zake na kuacha kukurupuka kuoana.

Fatma anasema ameolewa ndoa ya mitala ya wanawake wanne, yeye akiwa mke wa kwanza na anaishi vizuri wa wakewenza.

Fatma, aliyeolewa mwaka 2001 baada ya kumaliza chuo, anasema amefanikiwa kupata watoto watano.

Akizungumzia ukewenza, Fatma anasema tangu zamani unaonekana kama ni kitu kigumu, kinacholeta tafrani, uadui kwenye familia japokuwa kwa sasa imezidi.

Hata hivyo, katika mada anazozitoa anasema mapokeo ni mazuri na hii inaonyesha ni kwa namna gani lipo tatizo katika ndoa za aina hiyo, hasa kwa wakati huu ambao dunia imegubikwa na utandawazi.

Akieleza namna anavyoishi kwenye ndoa hizo za mitala, anasema kikubwa kilichomsaidia ni kuzaliwa na kulelewa kwenye familia yenye wakewenza.

“Ukewenza kwetu umeanzia kwa baba wa mama yangu, yaani babu yangu na waliishi nyumba moja na watoto hakuna ubaguzi,” anasema Fatma.

“Lakini hata baba yangu aliwahi kuoa wake wawili, baba zangu wadogo vilevile, hivyo ni maisha ambayo nilishayazoea na tulikuwa tukiishi kwa amani.”
Kwa upande wake, anasema mke mwenzie wa pili alipatikana wakati alipokwenda kusoma chuo Zanzibar mwaka 2006.

“Sababu mume wangu kuoa alisema hawezi kukaa mwenyewe kwa siku zote nitakapokuwepo masomoni. Hata hivyo, nashukuru katika hili mume wangu alinishirikisha, na kidini kukubali au kukataa kuolewa ukewenza haipo, isipokuwa mume anapaswa tu kukupa taarifa na wala sio hadi mwanamke kutoa ruhusa kwa kuwa ameshapewa ruhusa hiyo na Mungu na kukupa taarifa amekuheshimu tu,” anasema Fatma.

Akielezea maisha yalivyokuwa baada ya kuolewa mwenzake, anasema akiwa likizo alikuwa akienda kuishi naye nyumba moja, lakini alipomaliza chuo, ndio naye akatafutiwa nyumba yake.

Anasema mwaka 2015, mume wao huyo alioa tena mwanamke mwingine, lakini hakutaka kumuuliza sababu ya kuoa tena na ilipofika mwaka 2018 alioa tena mwingine na hivyo kufika wake wanne.

Akieleza namna wanavyoishi, anasema wanaishi kwa amani na hukutana kunapokuwa na matukio mbalimbali, ikiwamo ugonjwa, msiba au sherehe au mmoja akijifungua huwa wanaenda kumuona mtoto.

Pia, anasema wanakutana kwenye ‘group’ la WhatsApp la wanafamilia, huko hujadili mambo mbalimbali ya kifamilia wakiwa na ndugu wa mume pia na wanawake wengine walioolewa katika familia hiyo.

“Humo tunazungumza mambo mbalimbali ya kifamilia, tuna michango yetu ya shughuli mbalimbali za kifamilia,” anasema Fatma.

Pia, anasema huwa wanakuwa na kikao na mume wao kila anapoona inafaa na kuhusu kulala, mume ndio huwapangia siku moja moja kila mtu na wote wanaishi Kigamboni.

Anasema wakati yeye akiwa na watoto watano, mke wa pili ana watoto nne, watatu ana watoto wawili na wa nne ana watoto wawili.
 

Anachopaswa kufanya mwanamume

Fatma anatoa somo la namna mwanamume aliyeoa ndoa ya mitala anavyopaswa kuishi kuwa ni pamoja na kuwa mwadilifu kwa kumtendea haki kila mwanamke vile inavyotakiwa.

“Yaani kusiwe na upendeleo kati ya mwanamke mmoja dhidi ya mwanamke mwingine, huo ndio msingi wa kidini na migogoro mingi ndipo huanziaga hapo kwenye ndoa hizi za mitala,” anasema Fatma.

“Mfano mwanamume kwa mwanamke huyu atakwenda, kwa huyu haendi, kwa huyu anaenda siku tatu, kwa huyu mara moja, yaani hakuna utaratibu unaofahamika na hapo ndipo manung’uniko yanapoanza.

“Jingine mume anaweza kuonyesha mapenzi kwa huyu zaidi kuliko wengine, au anamtimizia mmoja au wawili kati yao mahitaji, mwingine hamtimizii, lakini kwetu nashukuru mume wetu anajitahidi kutimiza yote yanayotakiwa na pale inapotokea dharura hutoa taarifa na hiyo siku lazima afidie isipokuwa tu kama mwenyewe utaridhia kwamba zamu iendelee kama kawaida.”

Pamoja na ubusy alionao Fatma, hasa ziara za mihadhara na kwenda mikoa mbalimbali, anasema anaporudi huwa hadai siku ambazo hakuwa na mume wake, zaidi anaendelea pale mumewe anapokuwa ameishia.

Kuhusu watoto wao, anasema wanajuana, wengine wanasoma shule moja ambao ni wa mke wa pili na wa tatu.

Pia, anasema mtoto wake na wa mke wa pili walikuwa wanasoma shule moja ya msingi na sasa ndio wametengana baada ya kuingia sekondari.
Pia, anasema mume wao kitaaluma ni mwalimu, lakini kwa sasa anafanya biashara zake binafsi.


Mke kuwa mama wa nyumbani

Akizungumzia dhana ya wanawake wa Kiislamu kutakiwa kuwa nyumbani kulea watoto, Fatma anasema hili halina ukweli, isipokuwa anachotakiwa ni kazi anayoifanya isiathiri malezi ya watoto, kwa kuwa jukumu la kwanza la mwanamke kidini ni malezi kwa watoto.

“Shughuli yoyote halali mwanamke wa Kiislamu anatakiwa kuifanya kwa kuwa mwanamke anapaswa kutoa sadaka, anatakiwa kwenda Hija, ana wazazi wake anatakiwa kuwahudumia, vyote hivi hawezi kumtegemea tu mume. Mfano sadaka akikutolea mume atakuwa katoa yeye na sio wewe,” anasema Fatma.
 

Kurushana roho kwa wakewenza

Fatma anasema ukitaka kuishi katika ndoa hizi za mitala, ishi maisha yako na usijishughulishe na maisha ya mwenzio.

Anasema hata yeye huletewa maneno na watu mbalimbali kuhusu wake wenzie lakini kutokana na misimamo yake huwazima mapema.

“Usiwe mtumwa wa maisha ya wengine, kwa kufanya hivyo ndio utapata amani, lakini ukisema uchunguze maisha ya wengine kila siku utajikuta unakuwa mtumwa wa maisha ya mwingine badala yake ‘dili’ na mwanamume wako kwa kuwa ndiye aliyekuoa,” anasema Fatma.
 

Aonya wanaume

Wakati dini ikiruhusu wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja, Fatma anawataka kutotumia ruksa hiyo vibaya kwa kuwa kuna vigezo vyake, ikiwamo kuweza kuwahudumia hao wanawake.

“Lakini wanapaswa kuelewa kuoa wake wenza sio fasheni, bali kuwa na sababu inayomfanya aoe na kuwa na uwezo wa kuwahudumia, sio unaoa wake wote hao wakati hata mmoja uwezo wa kumhudumia huna,” anasema.
 

Sababu ndoa kuvunjika mapema

Katika hatua nyingine, Fatma anaeleza sababu za ndoa nyingi kuvunjika mapema, kuwa ni pamoja na watu kukurupuka kuoana.

“Baadhi wanakurupuka kuoa au kuolewa, wengine hawajui wajibu kama mke au mume ni upi na hata katika kuchagua hawafuati masharti na vigezo viliyowekwa,” anasema Fatma.
 

Mihadhara

Kuhusu kufanya mihadhara, Fatma anasema aliianza tangu zamani kwa kuwa alikuwa mwalimu wa somo la dini ya Kiislamu.
Anasema amesoma bailojia, jiografia na elimu ya dini ya Kiislamu, kwa hiyo ni mwalimu wa masomo hayo matatu.

“Hivyo ukiacha kusomesha darasani, huwa nasomesha pia darasa za kina mama kwa taaluma hii niliyonayo, mwaka 2002 nilipewa uongozi na Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania, moja ya majukumu ya baraza hilo ni kufanya mihadhara hii ya kidini na mabinti na ndipo nimejikuta nikifanya kazi hiyo hadi sasa, huku cheo changu kikiwa ni Hamirati wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kuhusu mgawanyo wa muda wa kufanya shughuli zake hizo, Fatma anasema huwa anajipanga kuwa shule kwa kuwa mihadhara hufanyika kwa mwezi mara moja.
Anasema labda itokee watu wamemualika, lakini mihadhara mingine huibuka kutokana na matukio, mfano ya mwaka mpya wa Kiislamu au kipindi cha Mfungo wa Ramadhani ambao huwaelimisha kinamama kuhusu umuhimu wa kufunga.
 

Historia

Fatma Mdidi alizaliwa mwaka 1979. Alisoma Shule ya Msingi Hananasif iliyopo Kinondoni, kabla ya kujiunga Shule ya Sekondari ya Forodhani alikosoma kidato cha kwanza hadi cha nne.

Baadaye aliendelea na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Tambaza.
Masomo yake ya chuo alisoma Chuo cha Ualimu Ubungo Islamic ngazi ya diploma na kumaliza hapo mwaka 2001, kisha kwenda kufundisha Shule ya Kirinjiku Islamic iliyopo Same, mkoani Kilimanjaro mpaka 2003 aliporudi Dar es Salaam kumfuata mumewe.

Akiwa Dar es Salaam, Fatma anasema alifundisha Shule ya Kunduchi Girls Islamic kwa mwaka mmoja, kabla ya mwaka 2004 kwenda kujiendeleza kimasomo ngazi ya digrii Chuo Kikuu Abdulrahman Al-Sumait, Zanzibar na kumaliza mwaka 2007.

“Mwaka 2008 nikafundisha Shule ya Kipata Girls Islamic iliyopo Kariakoo, lakini baadaye hawa walifungua chuo chao cha ualimu kilichopo Kigamboni na kunihamishia huko. Nilifanya kazi huko mpaka mwaka 2016,” anasema Fatma.

“Hata hivyo, kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2020 niliamua kuwa tu nyumbani kulea watoto baada ya kupata changamoto za wafanyakazi wa nyumbani.
“Mwaka 2020 ndipo nikapata kazi ya kusimamia shule hii ya Ihsan Islamic iliyopo Kigamboni maeneo ya Kisarawe2, nikiwa mlezi mkuu wa shule, kazi ninayoifanya hadi sasa.”