Mwanafunzi adaiwa kuuawa kwa kunyongwa Mtwara Mikindani
Muktasari:
- Tukio hilo limetokea jana Jumapili Juni 21, 2026 saa 11 jioni na kuacha majonzi kwa familia, ndugu na wakazi wa eneo hilo
Mtwara. Simanzi, hofu na maswali mengi vimetanda katika Mtaa wa Lilungu, Kata ya Likombe, Manispaa ya Mtwara Mikindani, kufuatia kifo cha mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi King David, Moreen Nyamajeje (9), anayedaiwa kuuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limetokea jana Jumapili Juni 21, 2026 saa 11 jioni na kuacha majonzi kwa familia, ndugu na wakazi wa eneo hilo.
Mauaji hayo yanakuja wakati Juni 8, 2026, watoto wengine watatu wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Kilimahewa wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi, walipotea wakiwa njiani kwenda madrasa na kukutwa wamefariki dunia kwa kunyongwa.
Watoto hao ni Kulwa Mohamed (7) na Doto Mohamed (7), wanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mitopitopi pamoja na Rehema Mohamed (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mpanyu.
Miili ya watoto hao ilipatikana kwa nyakati tofauti, huku miwili ikipatikana Juni 13, 2026 na mmoja Juni 14, 2026 yote katika Pori la Kijiji cha Kilimahewa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 22, 2026, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lilungu, Fatuma Ally amesema kabla ya tukio hilo, mtoto Moreen alikuwa akicheza na wenzake nje ya nyumba yao iliyopo katika Kambi ya Jeshi la Magereza Lilungu.
Ally amesema watoto hao walikuwa watano wakicheza pamoja wakati watu wasiojulikana walipofika na kuanza kuwaita mmoja baada ya mwingine kwa ishara.
Amedai kuwa, baadaye watu hao walimchukua Moreen na kutokomea naye eneo la Shamba la Magereza, ambako baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa na dalili za kunyongwa.
“Watu hao walikuwa wakiwaita watoto kwa ishara, mmoja baada ya mwingine. Ilipofika kwa Moreen waliondoka naye kuelekea porini. Baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa na dalili za kunyongwa,” amesimulia Ally.
Amesema mmoja wa watoto waliokuwa wakicheza na marehemu Moreen, ambaye ni ndugu yake, alitoa taarifa kwa mama yao kuhusu tukio hilo, jambo lililosababisha familia kuanza kumtafuta kwa kushirikiana na majirani na wakazi wa eneo hilo.
Ally amesema tukio hilo limeibua hofu miongoni mwa wazazi na walezi wa eneo hilo.
“Hili tukio limetushtua sana. Tunaziomba mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema kiongozi huyo.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Lilungu wamesema tukio hilo limeongeza hofu kuhusu usalama wa watoto wao na kuwataka viongozi pamoja na vyombo vya ulinzi kuongeza jitihada za kulinda usalama wa wananchi.
Mmoja wa wakazi hao, Zuhura Issa ametoa rai kwa viongozi wa Serikali ya mtaa na wananchi kwa jumla, kuongeza ulinzi wa watoto ili kuzuia matukio kama hayo kutokea.
“Tunaomba Serikali ya mtaa isaidie kuanzisha au kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuongeza usalama wa watoto wetu. Tukio hili limetuogopesha sana,” amesema Issa.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lilijiri jana, Juni 21, 2026, jioni.
Amesema mtoto huyo alichukuliwa na watu wasiojulikana kabla ya kupatikana akiwa amefariki dunia.
“Huyu mtoto alikuwa anacheza na wenzake, walikuwa watatu. Watu hao walipofika walimwita mtoto kisha kutokomea naye, baadaye walitelekeza mwili wake porini,” amedai kamanda huyo.
Kamanda Suleiman amesema Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira ya tukio hilo, chanzo chake, pamoja na kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Zawadi Bwanali akizungumza na Mwananchi baada ya taarifa ya Jeshi la Polisi, amethibitisha kupokea mwili wa mtoto huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Wakati huohuo, imeelezwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi, huku vikitoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi wa mauaji hayo kujitokeza na kushirikiana na Jeshi la Polisi.