Mwanafunzi afariki baada ya kuchapwa viboko

Muktasari:
- Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Samanga, iliyoko Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Sistus Aristid Kimario (7) amefariki dunia, baada ya kudaiwa kuchapwa viboko na mwalimu wake.
Rombo. Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Samanga, iliyoko Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Sistus Aristid Kimario (7) amefariki dunia, baada ya kudaiwa kuchapwa viboko na mwalimu wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Julai 17, mwaka huu, ambapo amesema baada ya mwanafunzi huyo kuchapwa viboko na mwalimu huyo, alianguka na kukimbizwa hospitali ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Kamanda Maigwa amesema Jeshi hilo linaendelea kumsaka mwalimu aliyemchapa mwanafunzi huyo ambaye alikimbia baada ya kubaini mwanafunzi aliyemchapa amefariki dunia.
"Jeshi la Polisi linamsaka mwalimu mmoja, jina tunalihifadhi kwa sababu za uchunguzi, ambaye amekimbia baada ya kubaini mwanafunzi wa darasa la kwanza aitwaye Sistus Kimario, aliyemchapa viboko huko Shule ya Msingi Samanga, amefariki dunia julai 17, 2023.”
Aidha Kamanda Maigwa amewataka wananchi kutii sheria bila shuruti kwani uhalifu katika Mkoa wa Kilimanjaro, hauna nafasi.