Mwanafunzi auawa kwa kushambuliwa na Mamba Sengerema

Muktasari:

Matukio ya mamba kushambulia watu kisha kuwaua na wengine kupata ulemavu wa kudumu wakati wanafanya shughuli za kibinadamu ndani na kando ya Ziwa Victoria yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara wilayani Sengerema.

Buchosa. Martha Marco (12) mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Buhama iliyopo Kata ya Buhama Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba alipokuwa akifua nguo zake kandokando ya Ziwa Victoria.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Aprili 28, 2023, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyachitale, Baraka Benka amesema tukio hilo limetokea Aprili 26, 2023 katika kijiji hicho wakati mwanafunzi huyo akifua nguo zake ambapo mwili wa mwanafunzi huyo umepatikana na kuzikwa leo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Buhama, Shimba Alex amesema mwanafunzi huyo alikuwa na uwezo darasani hivyo kifo chake kimewasikitisha sana.

“Alikuwa na uwezo mkubwa darasani, kifo chake kimeleta simanzi kubwa baada ya mamba kukatisha uhai wake,”amesema Mwalimu Alex.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amethibitisha taarifa hizo za mwanafunzi huyo kupoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba