Mwanafunzi kidato cha tatu ajiua kwa risasi Moshi, aacha ujumbe

Muktasari:

  • Robert Meier (17) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Mary Goreti iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amejiua kwa kujipiga risasi huku akiacha ujumbe akitaka mwili wake uchomwe.

Moshi. Robert Meier (17) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Mary Goreti iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amejiua kwa kujipiga risasi huku akiacha ujumbe akitaka mwili wake uchomwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza na Mwananchi kwa simu baada ya kupata taarifa hizo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema lilitokea usiku wa kuamkia juzi.

Akisimulia tukio hilo, Kamnada huyo alidai kuwa kabla ya mwanafunzi huyo kujiua, aliacha ujumbe wa maandishi ulisomeka mwili wake uchomwe na majivu yake yasafirishwe kwenda Marekani yakazikwe pembezoni mwa kaburi la baba yake.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, baba yake Robert alifariki dunia akiwa Marekani na mwili wake ulizikwa nchini humo.

Kamanda Maigwa alifafanua kuwa siku ya tukio saa 8 usiku wa kuamkia juzi huko Mwereni katika Kata ya Ngangamfumuni, mwanafunzi huyo alijiua kwa kujipiga risasi kifuani upande wa kushoto kwenye moyo na risasi hiyo ikatokea mgongoni.

Alisema alijiua kwa kwa kutumia bastola namba LXE 023 aina ya Glock iliyotengenezwa nchini Austria, inayomilikiwa kihalali na mtu aitwaye Boniface Kimario, mkazi wa Mwereni ambaye Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano zaidi.

Kamanda Maigwa aliwataka wamiliki wa silaha wanaozimiliki kihalali kuwa makini na utunzaji wa silaha hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.


Janga la dunia

Vifo vya vitokanavyo na watu kujiua wakiwemo wanafunzi. hasa wa vyuo vikuu, si la Tanzania pekee bali kote duniani. Baadhi ya vyuo vikuu vimefikia hatua ya hata kuwa na programu maalumu za kuzuia vifo hivyo.

Nchini Afrika Kusini kwa mfano, watu kati ya 6000 na 8000, wakiwamo wanafunzi wanakadiriwa kufa kila kwa kujiua.

Kutokana na hilo, bila shaka elimu, hamasa na misaada mbalimbali inatakiwa kutolewa shuleni vyuoni ili kulinda kundi hili muhimu katika jamii.