Prime
Mwanafunzi UDOM afariki dunia, waeleza ilivyokuwa
Mwonekano wa Jengo la Utawala la Udom. Picha ya Mtandao
Muktasari:
- Kwenye mitandao ya kijamii taarifa zilidai kuwa mwanafunzi huyo alifia ndani ya bweni kutokana kukaa muda mrefu bila msaada licha ya uongozi kupewa taarifa za ugonjwa mapema, jambo ambalo limekanushwa.
Dar/Dodoma. Mwanafunzi wa mwaka wa pili, wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Suzana Tyaba amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Jumanne, Juni 16, 2026.
Kifo cha mwanafunzi huyo wa Shahada ya awali ya Elimu katika Elimu ya Awali ndaki ya Elimu, kimeibua utata baada ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa kifo hicho kimetokana na mazingira duni ya huduma za afya na uzembe wa watoa huduma katika zahanati, jambo ambalo uongozi wa Udom umelikanusha.
Baada ya kifo hicho, kumekuwa na taarifa kuwa mwanafunzi huyo alifia ndani ya bweni kutokana na kukaa muda mrefu bila msaada, chuo licha ya uongozi kupewa taarifa za ugonjwa mapema.
Taarifa hizo zimedai gari la kubebea wagonjwa lilifika kwa kuchelewa wakati ambao mwili wa mwanafunzi huyo ulishafikishwa hospitali.
Taarifa hizo kutoka kwa wanafunzi zilieleza zahanati iliyopo katika ndaki hiyo hufungwa mapema hali inayowanyima wanafunzi nafasi ya kupata huduma za afya kwa ufanisi.
Hata hivyo, Uongozi wa Udom umetoa taarifa juu ya tukio hilo ikieleza mwanafunzi huyo alifariki dunia wakati akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Udom, Rose Mdami ilieleza kuwa kifo cha mwanafunzi huyo hakikutokana na uzembe wa zahanati au kuchelewa kwa gari la wagonjwa.
“Mwanafunzi Suzana Tyaba, mwenye namba ya usajili T24-03-14396, aliyekuwa akisoma Shahada ya awali ya Elimu katika Elimu ya Awali ndaki ya Elimu amefariki alfajiri ya Jumanne Juni 16, 2026 akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa kuendelea na matibabu,” imeeleza taarifa hiyo.
Mdami anasema awali mwanafunzi huyo alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa na aliruhusiwa kurejea chuoni Juni, 14, 2026 ili kuendelea na masomo baada ya hali yake kuimarika.
Kwenye taarifa hiyo anasema alfajili ya Jumanne Juni, 16 hali yake ilibadilika ghafla akiwa bwenini ambapo uongozi wa usimamizi wa wanafunzi ulianza jitihada za kumuwahisha hospitalini baada ya kupata taarifa na alifikwa na umauti wakiwa njiani kabla ya kufika hospitali.
“Hali ya mwanafunzi huyo ilibadilika ghafla akiwa bwenini, mara baada ya taarifa hizo kufikia uongozi wa usimamizi wa wanafunzi, gari la wagonjwa la chuo liliitwa kwa ajili ya kumwahisha hospitalini, kwa masikitiko makubwa alifariki wakiwa njiani kuelekea hospitalini,” amesema Mdami.
Kuhusu huduma za afya katika zahanati hiyo, amesema hutolewa kila siku kuanzia asubuhi hadi saa 3:00 usiku na chuo hicho kina magari ya wagonjwa yanayopatikana muda wote kwa ajili ya kuwapeleka wanafunzi kwenye vituo vya afya, ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa, CIVE na Hospitali ya Chuo iliyopo eneo la Social.
UDOM pia imetoa wito kwa jamii na watumiaji wa mitandao ya kijamii kupokea na kusambaza taarifa kutoka vyanzo sahihi vya chuo hicho kwa kuzingatia maadili katika utoaji wa taarifa hizo,ili kuepusha taharuki, hasira na maumivu kwa wahusika.
Mwili wa mwanafunzi huyo utasafirishwa kwenda Kijiji cha Muzye, Kata ya Muzye wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya mazishi baada ya ratiba ya wanafamilia na maandalizi kukamilika.