Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwandishi wa Mwananchi ashinda tuzo ya Hedhi Salama 2026

Herieth Makweta (katikati) akiwa ameshika tuzo aliyoshinda.

Muktasari:

  • Tuzo hizo zimetolewa wakati wa kikao cha makatibu wakuu na maofisa waandamizi wa sekta mbalimbali zinazohusika na huduma za hedhi salama nchini.

Dodoma. Mwandishi mwandamizi wa habari za afya wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Herieth Makwetta, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Hedhi Salama 2026 katika kipengele cha magazeti.

Herieth ametangazwa mshindi na kukabidhiwa tuzo hiyo leo Ijumaa, Juni 12, 2026, akiwa miongoni mwa washindi wanane waliochaguliwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Tuzo hizo zimetolewa wakati wa kikao cha makatibu wakuu na maofisa waandamizi wa sekta mbalimbali zinazohusika na huduma za hedhi salama nchini.

Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer, amesisitiza kuwa hedhi si ugonjwa bali ni mabadiliko ya kawaida ya kibayolojia yanayoashiria ukuaji na ukomavu wa msichana.

Akifungua kikao cha wadau wa hedhi salama Dk Laizer amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata huduma rafiki za hedhi salama, ikiwemo kuandaa mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa hedhi salama na vifaa vya kufundishia.

Dk Laizer, amesema mwongozo huo umeweka mkazo katika uboreshaji wa miundombinu rafiki kwa wasichana na wanawake, ikiwemo vyoo bora, vyumba vya kubadilishia taulo za hedhi, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na mifumo ya utunzaji wa taka zinazotokana na hedhi.

Aidha, amebainisha umuhimu wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bora za hedhi na kuendelea kutoa elimu ya kuondoa mila na desturi potofu zinazochangia unyanyapaa kuhusu hedhi.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabia na Mawasiliano kutoka UNICEF, Reginaldah Mpete, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuratibu afua za hedhi salama nchini.

Amesema ushirikiano wa wizara na mashirika ya maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi umechangia mafanikio yaliyofikiwa, ikiwemo kuandaliwa kwa mwongozo wa kitaifa wa hedhi salama na kuimarika kwa uratibu wa wadau.

Herieth Makweta akiwa ameshika tuzo aliyoshinda.

Mpete, amesema wadau wa maendeleo wamekuwa sehemu muhimu katika safari ya kuimarisha hedhi salama nchini, kuanzia kufadhili utafiti wa kwanza wa kitaifa uliobaini hali halisi ya hedhi salama hadi kusaidia mafunzo ya wakufunzi wa mwongozo huo na usambazaji wake katika mikoa mbalimbali.

Kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya Tuzo za Hedhi Salama 2026 iliyotolewa na Muungano wa Tanzania wa Afya na Usafi wa Hedhi (TMHHC), makala na habari ziliwasilishwa na wanahabari kutoka makundi manne ya vyombo vya habari ambayo ni redio, televisheni, magazeti na blogu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kazi za washiriki zilipimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa mada katika kuhamasisha afya na usafi wa hedhi, ulinganifu na nguzo nne za muungano huo, uwezo wa kufikia hadhira kubwa, pamoja na matumizi ya takwimu, maoni ya wataalamu na sauti za wananchi katika habari husika.

Naye, Mratibu wa Tuzo za Hedhi Salama, Oliver Kavishe, amesema lengo la tuzo hizo ni kuhamasisha wanahabari na watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuandika na kutangaza kwa kina masuala ya afya ya hedhi ili kuongeza uelewa wa umma na kuvunja mila potofu zinazohusiana na hedhi.

“Tuzo hizi zimekuwa kichocheo muhimu kwa vyombo vya habari kuendelea kuibua mijadala na kutoa elimu kuhusu afya ya hedhi, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wasichana na wanawake,” amesema.

Jopo la majaji liliongozwa na mwakilishi wa Wizara ya Afya, Rabia Ismail, likishirikisha wajumbe kutoka Tanzania Sanitation and Hygiene Consortium (TASACI), WaterAid, Msichana Initiative na sekretarieti ya TMHHC.

Katika tathmini yao, majaji walibainisha kuwa bado kiwango cha uandishi na utangazaji wa masuala ya afya ya hedhi nchini ni cha chini, hususan katika majukwaa ya mitandao ya kijamii, hali inayohitaji juhudi zaidi za kujenga uwezo wa wanahabari na kuhamasisha ushiriki mpana katika kuripoti masuala hayo.

Naye mshinid wa tuzo, Makweta amesema "Napokea tuzo hii kwa furaha na unyenyekevu mkubwa kwani ni heshima kwangu kutambuliwa kwa kazi ya kuhabarisha umma kuhusu afya ya hedhi, suala ambalo lina mchango mkubwa katika afya, elimu na ustawi wa wasichana na wanawake nchini,"

Amesema kuwa tuzo aliyopata ni matokeo ya ushirikiano wa wahariri, vyanzo vya habari, wadau wa afya na wasomaji ambao wameendelea kuamini na kuthamini kazi anayoifanya.

"Ninaamini bado kuna haja kubwa ya kuendelea kutoa elimu kuhusu hedhi salama, kupambana na unyanyapaa na kuhakikisha kila msichana na mwanamke anapata taarifa sahihi pamoja na huduma stahiki. Nitaendelea kutumia kalamu yangu kuibua changamoto, mafanikio na fursa zilizopo katika eneo hili muhimu la afya ya jamii," amesema.