Mwekezaji mwingine abisha hodi Bandari ya Dar

Muktasari:

  • Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa,amesema kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za mchakato wa majadiliano na mwekezaji mwingine kwaajili ya bandari ya Dar es Salaam, katika gati namba nane hadi 11.

Arusha. Mchakato wa kumpata mwekezaji mwingine kwaajili ya uendelezaji Bandari ya Dar es Salaam, umekamilika, huku Serikali ikisema muda wowote atatangazwa na kukatakabidhiwa kazi.

Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 6, 2023 na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, wakati akifungua mkutano wa 16 wadau wa uchukuzi unaofanyika jijini Arusha kwa siku tatu.

Mbarawa amesema kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za mchakato wa majadiliano na mwekezaji huyo kwaajili ya gati namba nane hadi 11.

"Jamani ieleweke Serikali bila sekta binafsi haitaweza hivyo kwa kulijua hilo gati namba nane hadi 11 hivi karibuni tutaipa sekta nyingine binafsi lakini sio DP World. Mchakato wake unaendelea na ukimalizika kampuni hiyo itawekwa hadharani na itapewa kazi ya kuendesha Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema hii ni baada ya mafanikio ya kumleta mwekezaji Kampuni ya DP World ambae tayari ameanza maandalizi na kwamba muda wowote kuanzia sasa ataanza kazi.

"Jambo kubwa la kujivunia ni kumleta mwekezaji katika bandari, ingawa kulikuwa na changamoto kubwa, nashukuru Watanzania tulishirikiana na tumefanikiwa. Leo DP World yuko bandarini na muda wowote ataanza kufanya kazi yake,“ amesema Profesa Mbarawa.

Awali Oktoba 22, 2022 Serikali ya Tanzania ilitia saini mkataba na kampuni ya DP world ya kuendesha shughuli kwenye bandari ya Dar es Saalam na Juni 10, mwaka huu Bunge lilibariki makubaliano hayo hatua ambayo ilileta changamoto kwa wadau na makundi mabalimbali mbalimbali ya kijamii.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Omary Kiponza akizungumzia madhumuni ya mkutano huo ni kuangalia sera, sheria na kanuni mbali mbali zinavyosaidia sekta ya uchukuzi na usafirishaji.

Amesema lengo jingine ni kutoa taarifa ya mafanikio na changamoto sekta iliyopitia na kuishauri Serikali cha kuboresha kuendana na mabadiliko ya maendeleo ya kiuchumi.