Mwenge wa Uhuru wamtaka RC Katavi kurejesha Sh163 milioni

Muktasari:

  • Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahili Nyanzabara amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi (RC), Mwanamvua Mrindoko kurejesha Sh163.9 milioni za maendeleo ya mfuko wa vijana  wanazodaiwa.



Katavi. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahili Nyanzabara amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi (RC), Mwanamvua Mrindoko kurejesha Sh163.9 milioni za maendeleo ya mfuko wa vijana  wanazodaiwa.

Nyanzabara ametoa agizo hilo leo Alhamisi Septemba 23, 2022 mara baada ya mwenge wa uhuru kuanza kukimbizwa mkoani Katavi baada ya kupokelewa katika shule ya msingi Mirumba halmashauri ya Mpimbwe ukitokea Mkoa wa Rukwa.

"Halmashauri zote tano zinadaiwa hii siyo utani, RC kabla mwenge haujaoondoka Katavi ziwe zimerejeshwa isipofanyika hivyo hautaondoka Katavi," amesema Nyanzabara na kuongeza:

"Naanza na halmashauri hii ya Mpimbwe, inadaiwa Sh48 milioni kabla sijaondoka hapa zirejeshwe na tunakoelekea wajipange mwenge ukifika ziwe tayari zimerejeshwa."

Kwa upande wake, RC Mwanamvua amesema mwenge wa Uhuru utakagua,kuzindua na kuweka mawe ya misingi katika miradi 39 yenye thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni.

Katika halmashauri ya Mpimbwe, Mwenge huo umekagua miradi minne ikiwamo uzinduzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 0.6, kuzindua klabu ya wanafunzi ya kupinga rushwa shule ya Majimoto na kuweka jiwe la msingi kituo cha afya Kasansa miradi ambayo  haikuingia dosari.