Mwenyekiti wa kijiji ajinyonga, Polisi wachunguza

Muktasari:

Mwenyekiti wa kijiji cha Somanga, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Geofrey Massawe (45) amejiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya kufungia ng'ombe aliyokuwa ameifunga juu ya mti wa mparachichi.

Hai. Geofrey Massawe (45), Mwenyekiti wa kitongoji Somanga mkoani Kilimanjaro amejiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya kufungia ng'ombe aliyoifunga juu ya mti wa mparachichi jirani na nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Simoni Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Alhamisi Novemba 3 ambapo amesema mwili wa Mwenyekiti huyo ulikutwa juu ya mti na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo chake.



"Tukio hili limetokea jana majira ya asubuhi ambapo mwili wa marehemu ulikutwa ukining'inia juu ya mtu wa mparachichi akiwa tayari ameshafariki, marehemu hajaacha ujumbe wowote lakini tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili ili kubaini chanzo chake," amesema Kamanda Maigwa.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaja jina lake, amesema ndugu yao hakuwa na tatizo lolote na kwamba siku ya tukio alichukua kamba kwa ajili ya kwenda kufungia majani eneo jirani na nyumbani kwake lakini hakurudi.

"Huyu ndugu yetu hakuwa na tatizo lolote, siku ya jana alichukua kamba kwa ajili ya kwenda kukata majani eneo ambalo sio mbali na nyumbani kama kawaida yake, lakini baada muda mfupi tulipata taarifa kwamba kuna mtu amejinyonga na tulipofika eneo la tukio tulikuta ni ndugu yetu.

 "Kama familia tukio hili limetuumiza sana kwa kweli, hatujui ni nini kilichomkuta huyu ndugu yetu maana alikuwa hana shida na mtu yoyote na mtu," amesema ndugu huyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Sawe, Penda kimaro amesema baada ya kupata taarifa za kiongozi mwenzake kujinyonga alifika eneo ambalo mwili huo ulipokuwa na kushuhudia mwili huo ambapo alipiga simu kituo cha polisi Bomang'ombe na kufika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo.

Mwili wa Mwenyekitu huyo umehifadhiwa katika Zahanati ya Masama kwa ajili ya taratibu za mazishi.