Mwenyekiti Wazazi akemea ‘uchawa’ CCM

Muktasari:
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Dar es salaam, Khadija Ally Said, amesema kwa kuzuia tabia hiyo kutasaidia kufanikisha utekelezaji wa dira ya jumuiya hiyo inayofanyiwa kazi ambayo inaangazia maeneo matano ambayo ni Elimu, malezi, afya, mazingira na uchumi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Dar es salaam, Khadija Ally Said amekataa tabia ya makada wa chama hicho kumsifu hovyo (uchawa), huku akiwataka wafanye kazi kwa ushirikiano bila kujiona miungu watu.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kufanikisha utekelezaji wa dira ya jumuiya hiyo inayofanyiwa kazi ambayo inaangazia maeneo matano ambayo ni Elimu, malezi, afya, mazingira na uchumi.
Hayo ameyasema Desemba 14 baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa kamati ya utekelezaji wazazi mkoa ambapo watu wanne walichaguliwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Khadija ametaka kazi inayoonekana kufanyika bila kujali nani atakayenufaika na kazi hiyo.
“Nilisema mimi siyo mwenyekiti wa uchawa, wa kusifiwa, mimi ni mwenyekiti wa kazi, tunategemeana katika nafasi zetu, tutakwenda kufanya kazi kubwa kama jumuiya ya wazazi katika elimu na malezi, tunachangamoto ya malezi,” amesema Mwanaidi.
Kuhusu changamoto ya malezi iliyopo ndani ya jiji la Dar es Salaam na uwepo wa vitendo vya ukatili amewataka viongozi hao kuwa mifano kwa yale wanayoyatenda.
“Malezi haya na maadili yaanze na sisi, sisi tuwe mfano, hatuwezi kuwa na kiongozi asiye na maadili, maadili yake ya mshike mshike tia maji tia maji, tunataka mtuongoze sawa na mtakayotenda na siyo viongozi Mungu ambao mtakalosema ninyi ndiyo lifanyike,tuwe na uongozi shirikishi,” amesema Khadija.
Amesema katika mkoa wa Dar e salaam kuna kata 102 na wilaya tano hivyo waaliochaguliwa wanatakiwa kuhakikisha wanafanya kazi kikamilifu.
Kwa upande wake Omary Ngurangwa ambaye ni mmoja wa waliochaguliwa katika kamati ya utekelezaji, amesema kama mdau wa elimu atahakikisha shule zinazosimamiwa na jumuiya hiyo zinakuwa katika hali nzuri.
“Mimi ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu nitatumia mchango kuhakikisha shule zetu zinafanya vizuri, tutatoa ushauri ili kuhakikisha zinarudisha hadhi ya jumuiya yetu,” amesema Ngurangwa.
Naye Mwanaisha Ally Soud ambaye ni mjumbe wa baraza Jumuiya ya Wazazi mkoa alisema licha ya kushindwa katika uchaguzi lakini uchaguzi ulikuwa wa haki.
“Sisi tuliobaki tushirikiane ili kuendeleza gurudumu hili.”