Mwigulu: Nachukia unyang’anyi wa haki za watu
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na wananchi wa Idofi, Makambako mkoani Njombe, alipoanza ziara yake ya kikazi leo Mei 2, 2026 katika mikoa ya Iringa na Njombe.
Muktasari:
- Asema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa vijana wengi wanaofanya kazi katika viwanda na makampuni wananyimwa stahiki zao kwa kucheleweshwa malipo au kutolipwa kabisa, hali inayowakatisha tamaa na kuathiri ustawi wao wa maisha.
Dar/ Iringa. Ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba mkoani Iringa imeibua matumaini mapya kwa wananchi waliokuwa wamekata tamaa ya kudai haki zao, baada ya kiongozi huyo kuonesha wazi kuchukizwa na kile alichokiita unyang’anyi wa haki za wanyonge.
Akizungumza Mei 2, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igowole wilayani Mufindi, Dk Mwigulu amesema kama msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali hataruhusu tabia ya kuchelewesha au kukwepa kulipa madai halali ya wafanyakazi na watoa huduma iendelee kushamiri.
Amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa vijana wengi wanaofanya kazi katika viwanda na makampuni mbalimbali wananyimwa stahiki zao kwa kucheleweshwa malipo au kutolipwa kabisa, hali inayowakatisha tamaa na kuathiri maisha yao.
“Hii tabia ya kuzoea shida za watu na kuchezea jasho lao haikubaliki. Haki za wanyonge si za kufanyiwa mzaha,” amesema Dk Mwigulu.
Katika kusisitiza uzito wa tatizo hilo, Waziri Mkuu ameitaja kampuni moja binafsi (jina linahifadhiwa) ya kuwa miongoni mwa zinazolalamikiwa kwa kudaiwa kuwadhulumu wananchi, akisema kampuni hiyo inadaiwa na mwananchi mmoja Sh28 milioni tangu mwaka 2021, pamoja na Sh9 milioni za wafanyakazi tangu Aprili 2024.
“Huyu anadai Sh28 milioni tangu 2021, lakini ukiwaona wanaendelea na maisha ya anasa, wanabadilisha magari na mavazi kila siku, wakati wanaodai wanateseka,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa kuwasaka wamiliki wa kampuni hiyo ili wajisalimishe na kulipa madeni hayo mara moja kabla hajamaliza ziara yake.
“Nimesema watafuteni walipe madeni yote wanayodaiwa sasa nirudi hapa nikute hawajalipa halafu tupimane ubavu, haya ni mambo ya kupuuza haki za watu na yanafanyika kwa makusudi kabisa,”amesema.
Akisisitiza dhamira ya Serikali, Waziri Mkuu amesema uzoefu unaonesha kuwa ucheleweshaji wa malipo mara nyingi si kwa kukosa fedha bali ni uzembe na kupuuza haki za watu.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na wananchi wa Idofi, Makambako mkoani Njombe, alipoanza ziara yake ya kikazi leo Mei 2, 2026 katika mikoa ya Iringa na Njombe.
Ametolea mfano tukio la mkoani Kilimanjaro ambapo wakulima wa kahawa walikuwa wakidai Sh400 milioni kwa zaidi ya miaka saba.
Amesema aliagiza walipwe ndani ya mwezi mmoja, lakini walitekeleza ndani ya wiki moja tu, jambo alilosema linaonesha wazi kuwa baadhi ya wadaiwa huchelewesha kwa makusudi.
“Hii inaonesha si kwamba hawana uwezo, bali ni kukosa uwajibikaji,” amesema.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara Igowole Waziri Mkuu ameubana uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kufuatia malalamiko ya kikundi cha Ibantu Group kinachodai malipo ya muda mrefu baada ya kutekeleza kazi ya ufyatuaji tofali.
Mmoja wa wanakikundi hicho amesema walifyatua tofali 16,600 kwa makubaliano ya kulipwa Sh250 kwa kila tofali, sawa na zaidi ya Sh39 milioni, lakini hawajalipwa tangu mwaka 2022.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumeteseka sana. Hatuna pa kukimbilia, tunaomba msaada wako,” amesema mwanakikundi huyo.
Wananchi wa wa Idofi, Makambako mkoani Njombe wakimskiliza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipowasalimiana wakati wa ziara yake ya kikazi leo Mei 2, 2026 katika mikoa ya Iringa na Njombe.
Malalamiko mengine yametolewa na fundi Christopher Mwangoka, anayedai Sh1.5 milioni kwa kazi ya ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Kibengu, ambapo sehemu ya malipo ilishafanyika, lakini kiasi kilichobaki hakijalipwa kutokana na mvutano wa utekelezaji wa mkataba.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu amesema haiingii akilini kwa taasisi ya Serikali kupokea kazi na kushindwa kulipa walioitekeleza.
“Sasa kwa nini hamjawalipa? Kama mlipokea tofali, kwa nini haki yao haijatendeka?” amehoji kwa ukali.
Amesema Serikali haiwezi kujificha nyuma ya makosa ya wachache na kuwanyima haki wananchi waliotekeleza majukumu yao kwa uaminifu.
“Serikali haiwezi kujificha nyuma ya makosa ya watu wachache na kuwanyima haki wale waliotekeleza wajibu wao,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza uongozi wa halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinalipwa mara moja kabla hajaondoka eneo hilo, akisisitiza kuwa hataki kusikia visingizio vya aina yoyote.
“Ita timu yako yote ya wataalamu, mkuu wa wilaya na wahusika wote, hakikisheni mnalipa sasa hivi. Sitaki kusikia watu wanazungushwa tena,” amesema.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na wananchi wa Idofi, Makambako mkoani Njombe, alipoanza ziara yake ya kikazi leo Mei 2, 2026 katika mikoa ya Iringa na Njombe.
Kauli hiyo imeibua shangwe kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo, wengi wao wakionesha matumaini ya kupatikana kwa haki yao baada ya miaka ya kusubiri.
Waziri Mkuu amesema hataki kusikia tena malalamiko ya aina hiyo, akionya kuwa atakaporudi anatarajia kupata taarifa kuwa wadaiwa wote wamelipwa.
Amesema maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa kuwanyima haki wale wanaochangia kwa jasho lao, huku akiahidi Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa haki kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonya watendaji wa Serikali wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kisingizio cha taratibu na vibali, akisisitiza kuwa kauli ya Rais ni maelekezo ya mwisho yasiyohitaji mjadala.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni ya mwisho. Msitafute kibali kingine tena. Kama Rais ameelekeza na ameahidi, hayo ni maelekezo hakuna mwingine wa kuombwa kibali,” amesema.
Kauli hiyo imekuja baada ya wataalamu kujaribu kueleza ucheleweshaji wa mradi wa barabara ya Mtwango hadi Nyololo kwa kutumia lugha za kitaalamu, jambo lililomkera Waziri Mkuu.
Amesema wataalamu wanapaswa kuacha kutumia istilahi ngumu zinazochelewesha maamuzi na badala yake kuharakisha utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi.
“Najua wataalamu wetu akitaka kukupiga anaweka viingereza vingi; mara ‘evaluation’, mara ‘adjustment’. Ndani ya wiki mbili nataka mkandarasi apatikane na kazi ianze mara moja,” amesema.
Kutokana na hilo, amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kuhakikisha mchakato wa kumpata mkandarasi unakamilika ndani ya muda huo bila kuchelewa.
Amesema hali ya barabara katika eneo hilo inachangia kudorora kwa shughuli za kiuchumi licha ya uwepo wa uzalishaji mkubwa wa mazao ya misitu na viwandani.
“Haiwezekani watu wazalishe kwa miaka mingi halafu mazao yao yashindwe kufika sokoni kwa sababu ya barabara mbovu. Hii si haki kwa wananchi,” amesema.
Maelekezo hayo yamekuja kufuatia maombi ya viongozi wa mkoa huo akiwemo Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile, aliyesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara ili kukuza uchumi wa viwanda na kilimo.
Kihenzile amesema hali mbaya ya barabara ya Mtwango–Nyololo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya eneo hilo lenye zaidi ya viwanda 25 na mashamba makubwa ya chai.
Mbunge huyo amesema maombi yote makuu ya wananchi wa jimbo lake na halmashauri hiyo yanahusu barabara.
“Ombi la kwanza ni barabara, la pili ni barabara, la tatu ni barabara, la nne ni barabara na la tano ni barabara,” amesema Kihenzile.
Amesema wananchi wa jimbo hilo si waombaji wa misaada bali wanahitaji miundombinu bora itakayowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.